Na PETER FABIAN- TARIME
Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameeleza ugumu wa kudhibiti bidha za magendo katika mpaka wa Sirari wilayani Tarime.
Wamesema ugumu huo unatokana na kuwapo gari moja tu katika ofisi yao, ambalo ni bovu hivyo wanashindwa kufanya doria.
Wakizungumza kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini, baadhi ya maofisa hao walisema maeneo ya wilaya za Rorya na Tarime yana njia za panya zaidi ya 23.
Kwa mujibu wa maofisa hao, njie hizo zimekuwa zikitumika kuingia na kutoka nchi jirani ya Kenya kwa njia ya magendo.
Wamesema katika Wilaya ya Rorya zipo njia zisizo rasmi zaidi ya tisa ambazo wamekuwa wakizifanyia doria maeneo ya ndani ya Ziwa Victoria na nchi kavu,
“Kudhibiti magendo kwa kutumia gari moja kunatupa wakati mgumu kwa sababu tunapopata taarifa ya watu kupanga kupitisha bidhaa katika maeneo hayo huwa tunakwenda na kufanya doria ikiwamo kuweka vizuizi vya upekuzi.
“Lakini wakati tukifanya hivyo Wilaya ya Rorya, utasikia Wilaya ya Tarime mnapigiwa simu kupewa taarifa za wafanyabiashara kupitisha malori yaliyobeba bidhaa za magendo.
“Sasa ukiacha kudhibiti Rorya ukaenda maeneo ya Tarime unatoa mwanya kwa watu kupitisha mizigo ya magendo,” alieleza mmoja wa maofisa hao na kuongeza:
“Wakati mwingine gari likiwa kwenye matengenezo hutulazimu kuweka vizuizi daraja la Mto Mara kuelekea Makutano Musoma huku maeneo ya Nyamongo na Borega ya Tarime kuelekea Wilaya ya Serengeti yakikosa udhibiti jambo ambalo inafaa Kamishina wa TRA alifanyie kazi.
“Serikali na Kamishina wa TRA Charles Kicheere waongeze magari matatu na maofisa wengine kuweza kudhibiti maeneo ya Wilaya za Rorya na Tarime.”
Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli akiwa katika ziara ya kazi wilayani Tarime aligusia kuwapo wafanyabiashara wanaotumia njia za panya kuingiza bidhaa za magendo.
Aliwataka maofisa wa TRA na taasisi nyingine kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kukaa imara kudhibiti magendo badala ya kuwasaidia wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza bidhaa na kukwepa kodi.