Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Semina za jinsia na maendeleo zinazoratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) zimeleta mabadiliko nchini kwa kuwezesha washiriki mbalimbali kujitambua na wengine kuanzisha taasisi.
Kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya TGNP yanayotarajiwa kuadhimishwa kuanzia Novemba 7 hadi 10, 2023 washiriki wa semina hizo wamekutana kujadiliana walivyofanikiwa, changamoto na kuweka mikakati ya kusonga mbele.
Wakizungumza Oktoba 18,2023 wakati wa kongamano lililofanyika katika ofisi za TGNP, baadhi ya washiriki wamesema semina hizo zimewawezesha kuwa na uelewa wa masuala mbalimbali kama ya uongozi na kuaminiwa katika jamii.
Mmoja wa washiriki ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Alliance Democratic Change (ADC), Innocent Siliwa, amesema semina hizo zimemjenga kujiamini na kupata fursa ya kuingia kwenye vyama vya siasa.
“Semina zimetusaidia kusonga mbele, tunachambua bajeti za Serikali, tulifundishwa kutengeneza sera ikanisaidia kuingia kwenye vyama vya siasa…niliteuliwa Naibu Katibu Mkuu ADC Taifa mwaka 2021,” amesema Siliwa.
Manufaa mengine ya semina hizo ni kuanzishwa kwa vituo vya taarifa na maarifa (KC) katika maeneo mbalimbali nchini ambavyo vimewezesha kuibuliwa kwa matukio ya ukatili katika jamii.
Wivina Alikadi (37) mkazi wa Majohe ambaye alifanyiwa ukatili na mumewe amesema kupitia Kituo cha Taarifa Majohe amepata uelewa wa masuala ya ukatili na pia amepata mtaji wa kufanya biashara ili kujikimu kimaisha.
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, amesema mtandao huo ulipoanzishwa ulilenga kuratibu majukwaa mbalimbali ambayo yataleta sauti za pamoja na kwamba jukwaa la kwanza lililoanzishwa mwaka 1996 ni GDSS.
“Kwa miaka yote hiyo semina za jinsia na maendeleo hazijawahi kukosekana na zinafanyika kila Jumatano, tumeona washiriki wakinoa uelewa wao kuhusu masuala ya jinsia na maendeleo.
“Washiriki wengi wameweza kuanzisha taasisi zao ambazo zimefanya kazi kubwa katika ngazi ya jamii, kwahiyo katika miaka 30 tunajivunia sana.
“Tutatengeneza chapisho ambalo litaonyesha jinsi jukwaa hili lilivyoleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu ili vizazi vijavyo vione umuhimu wa kuwa na majukwaa ya kuleta sauti za pamoja,” amesema Liundi.