Na Safina Sarwatt, Moshi
Halmashuari ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro inatarajia kujenga zaidi madarasa 22 na kuweka madawati 50 kwa kila darasa lengo likiwa ni kukabiliana na adha ya msogamano wa Wanafunzi kwenye chumba kimoja kupitia fedha za mfuko wa UVIKO-19.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ameyasema hayo leo katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo ambapo amesema wamepokea zaidi ya Sh million 440 kutoka mfuko wa UVIKO – 19.
“Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imeanza utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu wa kujenga madarasa 22 kupitia fedha za mfuko wa UVIKO-19 kwa lengo la kuondoa adha kwa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani kukosa nafasi kuendelea na masomo,”amesema Raibu.
Amesema tayari baraza la madiwani kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameshapata mkandarasi atakayejenga madarasa hayo na kwamba watakamilisha kwa muda unaotakiwa.
Mkandarasi wa kampuni ya Ravji ya mjini Moshi, Mhandisi Peter Muhushi ambaye amejitolea kujenga madarasa hayo amewataka wananchi na Watendaji wa halmashauri ya manispaa ya Moshi kumpa ushirikiano ili kukamilisha kazi hiyo kabla ya Desemba 15,2021.
Mmoja wa madiwani hao Deogratias Mallya amemshurukuru mkandarasi huyo kwa kukubali kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa madarasa 22 nakuahidi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo pale atakapohitaji msaada lengo ni kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.