Na MWANDISHI WETU,
KWA kawaida joto la mwili huwa nyuzi 37 (linapopimwa kwenye mdomo), linabadilika badilika kwa nyuzi moja au zaidi siku inapoendelea.
Hivyo, joto la mwili wako linaweza kuwa chini asubuhi na kuwa juu jioni, sehemu fulani inayoitwa hypothalamus, iliyoko chini ya ubongo, hudhibiti joto la mwili.
Homa hutokea wakati mfumo wa kinga unapotokeza vitu fulani katika damu vinavyoitwa pyrogen, labda unaposhambuliwa na bakteria au virusi, hiyo hufanya hypothalamus iongeze joto la mwili.
Taasisi ya Mayo ya Elimu na Utafiti wa Kitiba, inasema homa husaidia mwili katika kuondoa bakteria na virusi.
Virusi vinavyosababisha mafua na magonjwa mengine ya kupumua husitawi wakati wa baridi, homa kidogo inaweza kusaidia mwili kuondoa virusi hivyo.
Inaelezwa kuwa kamwe haifai kutibu homa kidogo kwani inaweza kudhoofisha kinga ya mtoto.
Dk. Al Sacchetti wa Chuo cha Marekani cha Madaktari wa Dharura, anasema mara nyingi homa si ugonjwa lakini inaweza kuwa dalili ya ugonjwa.
Hivyo, mtoto wako anapokuwa na homa unapaswa kuzingatia afya yake badala ya kuwa na wasiwasi kuhusu joto lake.
Hupaswi kumpa mtoto wako dawa akiwa na kiwango cha joto cha nyuzi joto 101 za Fahrenhaiti (38.3 za Selsiasi) ila tu ikiwa anaumwa au hupatwa na mpapatiko mara kwa mara.
Hata joto la mwili wake likiwa juu zaidi hilo si hatari, isipokuwa awe na mpapatiko au ugonjwa mwingine hatari.
Ni vizuri kufahamu iwapo anakula na kulala vizuri, anacheza vizuri, basi hahitaji matibabu yoyote.
 Kutibu homa ya kawaida  Â
Pamoja na hayo pia kuna namna ambavyo unaweza kufanya ili kuhakikisha unamsaidia mtoto wako kwa kufuata njia za kitaalamu.
Mara nyingi njia ambazo zimekuwa zikipendekezwa na madaktari ni pamoja na kuhakikisha chumba cha mtoto hakina joto.
Pia kumvisha mavazi mepesi, hii ni kwa sababu mavazi mazito yanaweza kuongeza homa.
Pia njia nyingine ambayo unaweza kuitumia kumsaidia mtoto ni kuhakikisha unampa vinywaji kama maji, maji ya matunda yenye maji mengi na supu, kwa sababu homa inaweza kumfanya apoteze maji mengi.
Epuka kumpa vinywaji vyenye kafeini kama vile kola au chai isiyo na maziwa kwani hivi vinaweza kumfanya  apoteze maji zaidi.
Ni vizuri pia kuhakikisha unaepuka vyakula ambavyo havisagiki kwa urahisi kwani homa hupunguza utendaji tumboni.
Mara nyingi mtoto hupewa dawa za dukani za kutuliza maumivu kama vile ‘acetaminophen’ au ibuprofen joto lake linapopita nyuzi 38.9 za Selsiasi.
Ni muhimu pia kufuata maagizo yaliyo kwenye kibandiko, kwa maana ya kwamba watoto walio na umri wa chini ya miaka miwili wasipewe dawa zozote bila idhini ya daktari.
Dawa za kupunguza homa haziui virusi hivyo, hazitibu mtoto mafua au magonjwa mengine kama hayo, ingawa zinaweza kupunguza maumivu.
Wataalamu wamependekeza kwamba watoto walio chini ya umri wa miaka 16 wasipewe Aspirini ili kutuliza homa, kwa kuwa inaweza kusababisha ugonjwa hatari wa Reye.
Njia nyingine ambayo inaweza kukusaidia kukabiliana na homa kwa mtoto ni kumwogesha, mweke ndani ya beseni yenye maji kidogo yaliyo vuguvugu na umwogeshe.
Pia ni muhimu kuomba ushauri kwa daktari iwapo unaishi katika maeneo ambayo watu huugua magonjwa kama kidingapopo, ebola, homa ya matumbo au homa ya manjano.
Kwa vyovyote vile, jambo unalopaswa kuzingatia ni kumpunguzia mtoto wako maumivu.
Hata hivyo, si kweli kwamba homa husababisha ugonjwa wa mfumo wa neva au kifo, japo homa inatisha wakati inaposababisha mpapatiko, mara nyingi inafifia baadaye.
Hata hivyo, kinga ni bora kuliko tiba, hivyo njia bora zaidi ya kumkinga mtoto wako na magonjwa ni kumfundisha kuhusu usafi.
Watoto wanapaswa kufundishwa kunawa mikono mara kwa mara, hasa kabla ya kula, baada ya kwenda kujisaidia, baada ya kuwa mahali penye watu wengi au baada ya kumshika mnyama.