MARAFIKI leo ni siku ya mwisho kabisa kabla ya kuingia mwaka mpya. Yatupasa tumshukuru Mungu kwa kutufikisha siku ya leo, lakini tuendelee kuombeana heri ili tuweze kuingia sote katika mwaka ujao, saa chache zijazo.
Tunaweza kuona ni muda mfupi sana, lakini kwa Mungu ni muda mrefu zaidi na kwamba lolote laweza kutokea. Kwa dua zetu kwa Mungu wetu, kwa hakika tunaweza kuvuka salama mwaka huu unaoelekea ukingoni.
Hongereni pia kwa kumaliza shamrashamra za Sikukuu ya Krismas salama nikiwa na imani kuwa mu wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida.
Kwa upande wangu nipo salama kabisa. Ikiwa una matatizo ya uhusiano au unahitaji kupanua zaidi uelewa wako katika ulimwengu huu wa mapenzi, vitabu vyangu maarufu vya uhusiano – Maisha ya Ndoa, True Love na Let’s Talk About Love vitakusaidia sana.
Nakushauri vitafute, vitaongeza kitu katika uhusiano wako. Baada ya hayo, sasa tugeukie katika mada yetu ya leo kama inavyosomeka hapo juu.
Leo tupo kwenye sehemu ya mwisho, ikiwa ni wiki ya mwisho pia katika mwaka huu wa 2016. Twende kwenye hitimisho la mada yetu.
KUWA MSHAURI, MFARIJI
Hakikisha kwamba mwanzo wa mapenzi ni muda muafaka kwako kumuonesha mapenzi ya kweli mwenza wako, kumfariji na kumsaidia kwa hali na mali pindi akikumbwa na matatizo, ni kati ya mambo muhimu yatayomfanya aamini kuwa ni kweli una mapenzi ya dhati na siyo tamaa ya ngono kwake.
Jitahidi uwe mshauri wake mkuu, kama ana tabia ambazo unadhani siyo njema, ni vizuri ukamshauri na kumweleza kwa kina madhara ya jambo ambalo anataka kufanya, ili aepukane nalo.
Kama utakuwa na hoja za kutosha anaweza akabadilisha maamuzi mabaya ambayo alitarajia kuyafanya hapo kabla.
Pia, kabla hujafanya jambo lolote, mwite kisha zungumza naye kuhusu mawazo na mipango yako huku ukihitaji naye akuambie anachofikiria katika mtima wake kabla ya wewe kufanya mambo hayo.
Kwa vyovyote vile, ataona kuwa unatambua thamani yake kama mwanandoa wako mtarajiwa, ndiyo maana unamwita na kumshirikisha kabla ya kufanya kitu chochote, hasa kinachohusu maendeleo ya maisha.
ZAWADI HUNOGESHA
Jitahidi kumtumia zawadi za aina mbalimbali; kadi, nguo za ndani na vitu vingine vyenye mvuto wa kimapenzi, nakuhakikishia ikiwa utamfanyia hayo, lazima uhusiano wenu utadumu.
Rafiki zangu, naamini kuwa mnaweza kudumu na wapenzi wenu kwa muda mrefu mpaka mkafikia hatua ya ndoa kama wote mtakuwa na nia njema.
Lakini haya yote ni baada nyie kuvuka vizingiti kadhaa ambavyo kwa njia moja ama nyingine mtaviepuka ili kuendelea kuwa bora zaidi katika uhusiano wenu.
Mada imesha. Usikose wiki ijayo kwa mada nyingine mpya ambayo itakuwa inafungua pazia la mwaka mpya.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, ameandikia vitabu kama True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani. Kwa sasa ameandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.