27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO MANANE YATAKAYOKUEPUSHA NA MARADHI

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


 

kulala-mapema-ni-njia-moja-wapo-ya-kukufanya-uwe-na-afya-njemaKUNA watu huwa hawana desturi ya kuugua mara kwa mara, tofauti na wengine ambao maradhi kwao ni kawaida.

Ili kuepuka maradhi ya mara kwa mara, kuna mambo mengi ambayo binadamu anapaswa kuyazingatia. Leo tutazungumzia siri nane ambazo watu wasiougua mara kwa mara huzingatia.

1. Kupata usingizi na mapumziko ya kutosha

Matokeo ya tafiti nyingi zilizofanyika katika sehemu mbalimbali duniani yanaonyesha kwamba, watu wanaopata usingizi wa kutosha huwa na furaha na afya bora.

Tafiti zinaonyesha kwamba kupumzika na kupata usingizi kwa saa nane na zaidi ni muhimu katika kudumisha afya, kuzuia magonjwa na kukupa furaha.

Kukosa usingizi na kutokupata mapumziko ya kutosha huchangia kupandisha kiasi cha homoni zinazosababisha msongo wa mawazo na matatizo chungu nzima ya kiafya.

2. Kufanya mazoezi

Tafiti zinaonyesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara huupa mwili kinga ya maradhi mbalimbali. Tafiti zinaonyesha pia kwamba, kujumuika kwa kushiriki katika michezo husaidia kuzuia tatizo la msongo wa mawazo na matatizo mengine ya kiafya.

Mazoezi yana faida lukuki, ikiwa ni pamoja na kuzuia magonjwa sugu kama vile kisukari na magonjwa ya moyo. Mazoezi pia huongeza kinga ya mwili na kuongeza kiwango cha homoni zinazoleta hali ya furaha mwilini.

3. Epuka pombe kupindukia

Mvinyo na na aina nyingine ya pombe ni salama endapo tu zitatumika katika kiwango kinachokubalika kiafya, tafiti zinaonyesha kwamba kiasi kidogo cha mvinyo huimarisha afya ya moyo, mapafu na misuli hivyo kumsaidia mnywaji kupata kinga na magonjwa sugu yasiyo ambukizi.

Watu wenye uwezo wa kudhibiti kiasi cha kilevi wanachotumia hufurahia vinywaji wavipendavyo huku wakizilinda afya zao.

Ikumbukwe kwamba, kiwango cha pombe kinachokubalika kiafya, kwa watu wengi huweza kuonekana ni kidogo hivyo kuwafanya kunywa kupindukia. Unywaji pombe kupita kiasi huweza kusababisha madhara mengi kwa afya na hata kuhatarisha maisha yetu.

4. Kujali unachokula

Chakula kinaweza kuwa dawa au sumu kwa maana ya kiasi na aina ya chakula. Kula chakula bora ni kitu muhimu katika kudumisha afya bora.

Matokeo ya tafiti yanaonyesha kwamba watu wanaojali wanachokula kwa kuzingatia kula chakula bora hujikinga na aina nyingi za magonjwa hivyo kuwa na afya bora na furaha tele.

5. Kuwa na mitazamo chanya

Hufanya kazi kwa ufanisi na bidii wakati huo huo hukubaliana na matokeo. Huwa na mategemeo ya mafanikio na furaha katika maisha. Hufurahia maisha na kutokufungwa na makosa yanayotokea katika maisha.
Huchagua ubora juu ya kiasi na kuto jilinganisha au kujishindanisha na watu wengine.

6. Kucheka mara kwa mara

Ziko tafiti nyingi zinazoonyesha umuhimu wa kutabasamu na kucheka katika kudumisha afya. Watu wanaotabasamu na kucheka mara kwa mara hujikinga na msongo wa mawazo hivyo kukaribisha furaha na afya katika maisha yao.
Tafiti zinaonyesha pia kwamba, watu hawa huishi maisha marefu
yaliyojawa na afya na furaha.

7. Kulala na kuamka mapema

Kulala kwa muda wa kutosha peke yake haitoshi. Tafiti zinaonyesha kwamba, kulala mapema na kuamka mapema ni muhimu katika kudumisha afya na kuleta furaha maishani.

Baada ya kufanya kazi wakati wa mchana, kwa kawaida miili huwa imechoke hivyo
kuhitaji mapumziko. Lakini pia huwa na nguvu na ufanisi mkubwa wakati wa alfajiri.
Kwa maana hiyo, ni muhimu kulala mapema ili angalau kutimiza saa nane.

8. Kunawa mikono mara kwa mara

Tabia ya kunawa mikono mara kwa mara husaidia kuzuia magonjwa mbalimbali.
Matokeo ya tafiti hizo yanaonyesha kwamba kunawa kwa kutumia sabuni hutukinga na magonjwa kama vile kuharisha, mafua na magonjwa ya tumbo.

Ziko tafiti zilizowafuatilia watu wenye tabia ya kunawa mara kwa mara na kuwalinganisha na wale wasio na tabia hiyo na kubaini kwamba wenye tabia ya kunawa mikono mara kwa mara huwa na kinga ya magonjwa ya mlipuko kwa asilimia mpaka tisini.

Wataalamu na wanasayansi wanatushauri kunawa kabla na baada ya kula chochote, pia kunawa tunapotoka msalani na hata tunapotoka sehemu zenye mikusanyiko ya watu.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mtandao wa Jamii Health.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles