Na ATHUMANI MOHAMED
TUPO katika sehemu ya pili ya mada yetu ambayo ni ndefu kutokana na umuhimu wake. Nilitamani kuandika wiki moja tu nimalize, lakini ni mada ndefu yenye maelezo na vipengele vingi ndiyo maana nimelazimika kuitoa kwa awamu.
Kama nilivyotangulia kusema wiki iliyopita, maisha yanategemea namna ambavyo umeanza. Mafanikio kwenye maisha hayatokei kama ajali. Lazima uyatengeneze mazingira ya kuwa na mafanikio kwenye maisha yako.
Ni kweli kuna wakati baadhi ya watu hujikuta wakiogelea kwenye mafanikio kutokana na bahati zao, lakini si sahihi sana kutegemea mafanikio yanayotokana na bahati. Kwanza weka mazingira mazuri, kisha bahati itafuata.
Ndiyo maana katika mada hii tunawazungumzia vijana. Kwanini vijana? Ni kwa sababu ndiyo muda mzuri wa kutengeneza mazingira ya kufanikiwa katika maisha yao yajayo.
Hii inamaanisha ikiwa kijana atashindwa kutengeneza mazingira mazuri ya kujiweka kwenye mafanikio, basi huko mbele ataishia kushangaa mafanikio ya wenzake.
Hawa ndiyo wale wanaoishia kusema: “Aaaah! Jamaa usimuone vile, nimesoma naye yule,” mwingine atasema: “Yule brother anayepita na lile gari kali, nilisota naye sana kitaa,” na maneno mengine kama hayo.
Ukweli ni kwamba kusoma na mtu mwenye mafanikio hakukupi mafanikio au kufahamiana na mtu uliyesota naye mtaani, hakukusogezi wewe kwenye mafanikio bali juhudi zako binafsi na kutengeneza mazingira ya kufanikiwa tangu awali.
Wiki iliyopita tuliona mambo matatu ya kwanza ya muhimu kufanywa na kijana, leo tunaendelea na mada yetu katika vipengele vinavyofuata.
4. UFAHAMU KUHUSU MWENZI
Namzungumzia kijana mwenye uchu wa mafanikio. Mwenye ndoto za kuishi maisha ya kupendeza. Ni wazi kuwa katika maisha, muunganiko katika ndoa ni jambo la msingi na muhimu.
Ilivyo ni kwamba, ikitokea ukakosea kufanya uchaguzi sahihi wa mwenzi wa maisha yako basi kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kuharibu maisha yako kwa ujumla.
Ni vizuri ujifunze kwa undani kuhusu mwenzi wa maisha. Penda kuhudhuria semina zinazofundisha kuhusu mchumba na mwanandoa sahihi. Shiriki kikamilifu kwa wataalamu wa mambo ya uhusiano na hata wale wa kidini.
Kwa kupitia imani ya dini yako, shiriki kikamilifu semina na makongamano ambayo yatakujenga ufahamu kuhusu mwenzi sahihi wa maisha yako. Ukiwa na uwezo wa kumjua mwenzi sahihi, bila shaka utakuwa na maisha mazuri yasiyo na matatizo kwenye uhusiano.
Ni dhahiri bila shaka yoyote, ukiwa na mwezi sahihi na ukatulia, utakuwa na utulivu wa akili utakaokufanya ufikiri vizuri zaidi juu ya namna gani unaweza kufanikiwa maishani mwako.
Hutakuwa sawa na yule anayewaza kuhusu kutatua matatizo ya uhusiano wake badala ya maendeleo ya maisha.
5. MCHUMBA BORA
Kwa kutumia utaalamu uliojifunza katika kipengele kilichopita, sasa hapa unatakiwa kutafuta mchumba bora. Bila kujali jinsia, kuwa na mchumba sahihi ni muhimu kama kuwa na mwanandoa sahihi kama nilivyotangulia kusema katika kipengele kilichopita.
Muhimu kwako, hutakiwi kuchanganya mchumba na mwanandoa. Unaweza kuwa na mchumba bora, ukaamini ni bora lakini asiwe mwanandoa bora!
Wakati mwingine unaweza kuwa na mchumba ambaye unadhani hayupo sawa, lakini kumbe ndiye mwanandoa sahihi.
Yote kwa yote, kumpata mchumba bora ni mwanzo wa kumpata mwanandoa bora na sahihi pia.
6. OMBA MWANANDOA
Huwezi kumpata mwenzi wa ndoa kwa uwezo wa kawaida wa akili zako mwenyewe. Katika hili mshirikishe Mungu. Kwa kutumia imani yako ya dini unayoamini, omba sana kwa Mungu akupe mke au mume mwema wa maisha yako.
Kumbuka unaweza kupata mchumba bora lakini si mwanandoa bora. Usisahau kuwa kuingia kwenye muunganiko usio sahihi wa ndoa inaweza kuwa kichocheo cha kuharibu mipango ya maisha yako.
Ndiyo maana inaelezwa kuwa, nyuma ya mafanikio ya mwanamume kuna mwanamke makini. Geuza msemo huo kwa mwanamke, utapata maana hiyohiyo.
Wiki ijayo tutaendelea na somo letu, USIKOSE!