25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO 20 YA KUZINGATIA UKIWA KIJANA

Na ATHUMANI MOHAMED

MATATIZO mengi yanayotokea kwa binadamu, husababishwa na mwanzo mbaya wa mipango ya maisha yake. Ni asilimia ndogo sana ya matatizo hutokea kwa bahati mbaya tu kutokana na sababu za hapa na pale.

Lakini mengi kati yao, husababishwa na kwenda ilimradi siku zinakwenda. Wale wanaopanga mambo yao mapema, huwa hawana kitu kigeni kwenye maisha yao. Kila kitu kinachotokea huwa kwa sababu tayari walishajipanga kabla hakijatokea.

Binadamu makini mwenye mafanikio na afya njema, pamoja na mambo mengine, husababishwa na umakini wake katika hatua na mapito ya maisha yake. Ukiweza hayo, maisha yako yatakuwa rahisi.

Hata hivyo kwa bahati mbaya au kwa kutokujua, wapo ambao wanakosea sehemu za hatua za maisha jambo linalosababisha baadaye waharibu kabisa maisha yao.

Katika mada hii nitaeleza mambo 20 yale ya muhimu zaidi ambayo kijana anapaswa kuyajua ili maisha yake yawe bora.

Kwa hakika mambo haya, kama yakizingatiwa bila shaka kijana atakuwa amejenga msingi imara wa maisha yake na kwamba huko mbele atakuwa mjuzi wa mambo mengi, akiwa na maarifa chanya yatakayomjenga kwenye maisha yake.

  1. UTII WAZAZI

Hili ni jambo la msingi sana, uzuri ni kwamba jambo hili limeelekezwa hadi katika vitabu vya dini. kwamba watoto wana wajibu wa kuwaheshimu na kuwatii wazazi wao.

Heshima kwa mzazi kuna faida nyingi, utakuwa na hakika ya kupata radhi zao, hivyo kuwa na uhakika wa kuishi maisha bora.

Waswahili wana msemo usemao: “Asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu.”

  1. IMANI YA DINI

Hofu ya Mungu ni kitu cha muhimu sana katika maisha. Lakini huwezi kuwa na hofu kama ukiwa huna imani. Inawezekana unayo imani yako kiasili, lakini usiwe mshirika mkamilifu wa imani hiyo.

Katika maisha ni kosa. Kuijua, kujifunza, kuifuata, kuitii na kuipenda imani yako itakusaidia sana maishani. Mtu mwenye kuifuata imani yake, bila shaka atakuwa mbali na vitu vibaya.

Ukimjua Mungu hutaiba, hutasema uongo, hutadhulumu wala kufanya mambo mengine yanayofanana na hayo ambayo kimsingi si ya kuwapendeza hata binadamu wenzako.

Msingi wa yote hayo ni kwamba utakuwa kioo kwenye maisha na hapo utapata marafiki wengi watakaokusaidia kutimiza ndoto za maisha yako.

  1. KUFUNGAMANA NA JAMII

Mafanikio ya maisha yana uhusiano mkubwa sana na namna unavyoishi na jamii inayokuzunguka. Ikiwa utaishi kipeke yako kwa kila kitu, jamii itakutenga.

Mazoea haya huanzia katika kipindi cha ujana. Lazima kijana atengeneze wigo mpana wa kuwa mshirika mkubwa kwenye mambo mbalimbali ya kijamii.

Kufanya hivyo kutakusaidia sana kusaidika pale unapokuwa na matatizo. Shiriki kwenye shughuli za kijamii, mfano msiba, sherehe nk. Kujichanganya kwako kutakuweka karibu zaidi na jamii inayokuzunguka.

Muhimu zaidi ni kwamba, utakuwa sehemu ya jamii na siku zote tunasema mtaji namba moja kwenye maisha ni watu. Ukiwa na watu hesabu maisha yako ni rahisi.

Ni kweli vitu muhimu ni fedha, wazo na watu, lakini cha kwanza kati ya vyote ni watu.

Kwa leo naishia hapa. Wiki ijayo tutaendelea na sehemu inayofuata, USIKOSE!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles