23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NAY WA MITEGO ALIVYOLINDWA KIBABE ZANZIBAR

Na FESTO POLEA, ZANZIBAR
WAKATI wimbo wa ‘Wapo’ wa rapa Emmanuel Elibariki (Nay wa Mitego) ulipotoka, kilichofuata ni hofu ya kukamatwa na kushtakiwa kufuatia ujumbe uliopo ndani yake, kweli alikamatwa lakini hakushtakiwa.

Kauli ya Rais Magufuli kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ya kwamba msanii huyo aachiwe huru na wimbo uendelee kuchezwa kwenye vyombo vya habari, kwa haraka ilibadili mawazo ya rapa huyo aliyeiona fursa ya kutengeneza fedha kupitia ngoma hiyo.

Ajipanga kuzunguka Tanzania

Baada ya kugundua kwamba shoo ndizo zinazomlipa zaidi, Nay ameamua kuandaa maonyesho mengi atakayoyafanya mikoa 11 ya Tanzania Bara, akianza na Iringa pamoja na Arusha.

Swali ni kwamba, ni namna gani ataweza kufanikisha shoo hizo kwenye mikoa yote huku akidai ameingiwa na hofu ya maisha yake kutokana na kupokea vitisho kwa wasioupenda wimbo huo?

“Kwa sasa maisha yangu yanazungukwa na wabaya wengi, tangu nitoe wimbo huu ulipokelewa vyema na watu wengi, lakini wapo wanaouchukia, nadhani ndio wanaonipigia simu za vitisho, lakini siwezi kunyamaza, nitaendelea kusema ukweli,

 “Kwa kuwa napenda ujumbe uliopo kwenye wimbo huu ufike kwa watu wangu, nitaanza ziara ya mikoani, nikianzia Iringa na Arusha, kisha nitazunguka mikao mingine 11 na huko kote nitakuwa nikilindwa na walinzi wangu,’’ anaeleza Nay wa Mitego.

Safari ya Zanzibar
Nay alipopata mwaliko wa kushiriki kwenye Tamasha la Muziki na Utamaduni, Zanzibar Swahili, anasema alichofikiria kwanza ni usalama wake, ndiyo maana kwenye mkataba wake aliomba kupewa ulinzi wa uhakika wakati wote atakapokuwa Zanzibar.

Maombi hayo yalikubaliwa na uongozi wa tamasha kwa kumpatia hoteli ya uhakika na ulinzi wa kutosha kwa kipindi chote alichokuwa kisiwani humo.

“Kweli Nay alituomba ulinzi, alitaka apatiwe mabaunsa wawili na askari polisi mmoja, nasi tulimpatia kama alivyotaka maana ndivyo tulivyokubaliana kimkataba,’’ anasema Joseph, meneja wa Tamasha la Zanzibar Swahili.

Ajali ya gari
Mashabiki wake walipopata taarifa kwamba angekwenda Zanzibar kwa ndege majira ya saa tano, walifika uwanja wa ndege kwa lengo la kumpokea, lakini baadaye walipata taarifa kwamba msanii huyo hatafika muda huo kutokana na kupata ajali ya gari wakati alipokuwa akielekea uwanja wa ndege, Dar es Salaam.

“Tulipokea taarifa kwamba Nay amepata ajali ya gari alipokuwa anakwenda Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, hivyo asingefika saa tano na atafika jioni,’’ alieleza mmoja wa viongozi wa tamasha hilo.

Ulinzi jukwaani
Namna alivyolindwa Nay ni tofauti na wasanii wote waliofanya shoo siku ile, ulinzi wake uliwashangaza wengi, kwani hata matarajio ya mashabiki kupiga naye picha hayakufanikiwa.

Nay aliingia ukumbini hapo akiwa amezungukwa na mabaunsa zaidi ya saba pamoja na idadi kubwa ya wapambe wake kiasi kwamba hakuweza kuonekana na watu alipokuwa akipanda jukwaani.

Alipomaliza kufanya onyesho yake alizungukwa tena na walinzi hao tangu akiwa jukwaani hadi alipofikishwa kwenye gari, aliingizwa kwa kasi kisha gari kuondoka.

 “Tangu nilipokamatwa na polisi kutokana na wimbo wangu wa ‘Wapo’ nimekuwa nikifanya shoo zangu na ulinzi wa kutosha kwa kuwa nahitaji kulindwa, maana peke yangu sitaweza,
“Hivi karibuni kabla ya Tamasha kubwa la Zanzibar nilifanya onyesho Singida, huko nilikuwa nikilindwa na walinzi wangu ninaokuwa nao muda wote tangu nilipotoa wimbo huu,’’ anasema Nay.

Asepa na kijiji Zanzibar

Kabla ya kuimba wimbo wa ‘Wapo’ Ney alianza kwa kutoa ujumbe kwamba hatanyamaza, atapaza sauti kwa anachoona ni sahihi na haki kwa watu wake bila kuogopa simu za vitisho anazopigiwa na watu asiowajua.

“Mimi siwezi kukaa kimya, nitaendelea kuwa mtetezi wenu wakati wote na kudhihirisha hili Dj lete ngoma,’’ alimweleza Dj apige wimbo wa ‘Wapo’, ukapigwa na hali ukumbini hapo ikabadilika ghafla, kelele za shangwe zikaongezeka na kusikika kelele za wapo, wapo, wapo na kila shabiki aliimba naye mstari mmoja baada ya mwingine.

Kwa nini Nay anajilinda
Kwa madai ya Nay wa Mitego ni kwamba ameamua kulindwa kwa sababu toka alipotoa wimbo huo amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu wasiofahamika. Wakati mwingine anatokewa na vitu vya kuhatarisha maisha yake, jambo linalomtia hofu.

 “Naamini wimbo huu una mashabiki wengi, lakini pia wapo wengi hawapendi sijui malengo yao, lakini kama wananipigia simu za vitisho, lengo lao si jema kwangu, ndiyo maana nalinda usalama wangu kokote niendako,’’ anasema Nay.

Ney anasema anafanya hivyo kwa kuwa maisha yake kwa sasa hayana amani kwa asilimia kubwa, hivyo kila anapokuwa kwenye shoo zake huwa na ulinzi mkubwa wa polisi pamoja na mabaunsa wa kutosha wanaohakikisha usalama wake kwanza ndipo apande jukwaani, tofauti na hivyo hafanyi shoo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles