Mwandishi Wetu
Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, amesema Wilaya ya Mwanga ilikuwa haiendelei kwa sababu uongozi hauko sawa hadi kufikia hatua ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya kupigana ofisini.
Amesema hayo leo Jumanne Januari 29, Ikulu jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kuapishwa kwa majaji wapya wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya walioteuliwa na Rais John Magufuli, Januari 27, mwaka huu.
“Haya mambo yanayoendelea hayawiani na maadili ya uongozi, kule Mwanga watu wanapigana magumi maofisini sasa hivi.
“Wilaya nzuri lakini sasa hivi haiendelei kwa sababu uongozi hauko sawa. Kule Tarime kuna rushwa DC mpya usiende kurudia yaliyotokea,” amesema mama Samia.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Charles Kabeho, kukomesha unyanyasaji wa kijinsia wilayani humo.
“Kuna mambo ya unyanyasaji sana huko hasa kwa watoto wa kike, nenda ukazingatie zile mila na desturi mbovu ukaziondoe nzuri zibaki,” amesema.