Na ESTHER MNYIKA-ALIYEKUWA SINGIDA
KUMEKUWAPO na ongezeko kubwa la watu wasiojiweza kuomba katika miji na majiji hapa nchini kutokana na jamii zinazowazunguka kutowasaidia.
Ongezeko hilo limesababisha kuanzishwa kwa vituo vingi vinavyohudumia wazee wasiojiweza, yatima na wengineo.
Katika vituo hivyo wamekuwa na changamoto mbalimbali zikiwamo kukosekana kwa mahitaji muhimu kama chakula na mavazi.
Hali hiyo imesababisha wazee hao kutoka kwenye vituo au kambi zao na kwenda barabarani kuomba omba ili waweze kupata fedha za kujikimu, jambo linaloongeza wimbi la ombaomba mitaani.
Taasisi za serikali na zisizo za kiserikali zimekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wazee na yatima kwa kutoa msaada wa chakula na mavazi, lakini kuna changamoto ya baadhi ya viongozi na wahudumu wa watu hawa kukosa uaminifu kwa kutowafikishia walengwa badala yake wanachukua wao.
Hivi majuzi, Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli na Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa walifanya ziara ya kutembelea kambi za wazee wasiojiweza, wenye ugonjwa wa ukoma na walemavu na kutoa msaada wa vyakula katika mikoa ya Singida na Tabora.
Katika ziara hiyo, walianza kwa kuwatembelea wazee wa Kituo cha Sukamahela kilichopo Kata ya Solya katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida. Katika kituo hicho wamekabidhi jumla ya tani 7.5 za vyakula.
Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1974 na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa ajili ya wazee waliougua ugonjwa wa ukoma na wazee wasiojiweza.
Baba wa Taifa alijenga nyumba katika kituo hicho na aliitaka Serikali iwahudumie wazee hao kwa kila kitu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo ukiwamo mchele, unga na maharagwe, Mama Janeth anasema kuna changamoto nyingi katika kuhudumia wazee hivyo wanahitaji ushirikiano wa hali na mali.
Anasema alitoa agizo kwa viongozi wa kituo kuhakikisha chakula hicho hakichakachuliwi na kiwafikie walengwa kwa sababu hao wazee wamezeeka hawana nguvu za kutafuta wala kulima, ndio maana wapo kambini ili wapate msaada.
Anataja idadi ya kilo za vyakula hivyo kuwa ni mchele kg 3,125; unga kg 3,125 na maharagwe kg 1,250.
“Vituo hivi vinavyo hudumia wazee vipo nje ya mkoa inakuwa si rahisi kuhudumia ipasavyo kwa sababu wadau wanakuwa wanashinda kutoa msaada kutokana na umbali wa vituo hivyo.
“Tuwasaidie wazee hawa kwa sababu nasi ni wazee watarajiwa, tutahitaji msaada kama hawa nawaomba wadau, taasisi, wafanyabiashara na wananchi tushirikiane ni jukumu letu wote,” anasema Mama Janeth.
Aidha, aliwaomba Watanzania kujenga tabia ya kusaidia watu wasiojiweza na wenye mahitaji maalumu.
Pia, alimshukuru Mhubiri kutoka nchini Nigeria, Temitope Balogun Joshua maarufu (T.B Joshua) kwa kuwa mfadhili wa suala hilo na wamekuwa pamoja.
Kwa upande wake, Mama Mary aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wazee wanaoishi katika makazi ya kulelea walemavu na wasiojiweza nchini kwa sababu wanakabiliwa na changamoto nyingi.
“Watanzania wote popote mlipo tukumbuke kutembelea vituo vya kulelea wazee kikiwamo hiki tulichokitembelea cha Sukamahela na kutoa misaada kwa kadri mtakavyojaaliwa,” anasema Mama Mary.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Mlata anasema kutokana na juhudi za mama Janeth kwa kutambua umuhimu wa wazee wanamuunga mkono kwa kutoa msada wa vyakula vyenye thamani ya Sh milioni 2,198,460.
Anavitaja baadhi ya vitu vingine walivyotoa kuwa ni soda, maji, mafuta ya kula na sukari.
Naye Mkuu wa kituo hicho, Jeremia Muho anasema kituo kilianzishwa mwaka 1974 kikiwa na ukubwa wa eneo lenye hekta 80 hadi sasa wamefanikiwa kujenga nyumba 52.
Anasema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuhudumia wazee wanaougua ugonjwa wa ukoma na wasiojiweza.
“Kituo hiki hadi sasa kina jumla ya wazee na watoto 62 ambapo wanaume 22, wanawake 23 watoto wa kiume watano na wakike 12 idadi ambayo kwa sasa imepungua,” anasema Muho.
Anasema kuwa wazee saba kati ya wanane wana matatizo ya macho kuona kwa sasa wamefanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri.
Anataja changamoto zinazowakabili kuwa ni mpishi kuwa mmoja hivyo kusababisha wazee hao kula mlo mmoja kwa siku. Hivyo, wanahitaji kuongezewa wapishi kwa ajili ya kuhakikisha wazee wanapata milo mitatu.
Anataja changamoto nyingine kuwa ni nyumba zimechakaa na ukosefu wa huduma ya nishati ya umeme hivyo wanaiomba Serikali na wadaua kuwafanyia ukarabati wa mazingira.