NA AZIZA MASOUD
KILA mtu ana taratibu zake katika malezi ya mtoto kuanzia anapozaliwa na kadiri anavyoendelea kukua.
Ndio maana utakuta tabia zinatofautiana kwa kila mtoto kuwa na tabia za pekee, achilia mbali zile za kuzaliwa nazo.
Suala la tabia ya mtoto aliye chini ya miaka 18 huchangiwa na malezi ya wazazi/mzazi/mlezi kulingana na vile alivyozoea kufundishwa ama kuelekezwa.
Leo nazungumza na wazazi ambao wamezoea kudekeza watoto. Unakuta mtoto anadeka hadi anakera.
Kudekeza mtoto si malezi bora kwani humfanya mtoto kujiona mtoto kila kukicha na anaweza kujibu au kulia kila wakati hata kwa jambo lisilokuwa na msingi, kwa sababu hajazoea kuonywa wala kufundishwa tofauti na anavyofanyiwa.
Unakuta mtoto mwingine anacheza na wenzake wa rika moja lakini cha ajabu kila mara ni yeye anayelia, ukiuliza sababu unaambiwa analilia kitu fulani, ni malezi mabaya ndio yanachangia.
Mtoto kama huyo hata akiwa mkubwa, atakuwa hawezi kujisimamia hata kwa baadhi ya mambo ya msingi kutokana na namna mzazi/mlezi ulivyozoea kumdekeza.
Katika malezi unapaswa si tu kuwa mkali, bali kutumia busara na kuangalia namna bora ya kumjenga mtoto wako katika njia sahihi ya kumjua Mungu, kuwa na heshima na jinsi ya kuishi na jamii inayomzunguka.
Hili halijalishi kama maisha yako hayaingiliani na jamii inayokuzunguka, lakini unaweza kumjenga mwanao kwa kutumia baadhi ya ndugu wa karibu wanaokuja nyumbani kwako kwa kumwelekeza namna ya kuishi na jamii.
Pia mtoto hujifunza haraka kupitia wazazi wake, unapofanya jambo kuwa makini nalo kwa kuhakikisha kuwa ni sahihi kwani inakuwa tayari umeacha alama kichwani kwa mwanao kwa hicho kilichofanyika.
Mfano, namna unavyozungumza na mlezi wa mtoto wako nyumbani, kama humchukulii kuwa ni mmoja wa wanafamilia, tegemea hata mtoto atamchukulia hivyo hivyo.
Mzazi/mlezi unapaswa kufahamu kuwa huyo ni mwanao, lakini pia ni mume au mke wa mtu mtarajiwa, ni padre au mchungaji mtarajiwa, ni Daktari/ Muuguzi, Mwalimu n.k hivyo mtengeneze vyema ili kumsaidia kuishi bila tatizo kwenye jamii.