32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MALAIKA ASIMULIA ZIARA YA MAREKANI, KOLABO NA BIEBER

Na JOHANES RESPICHIUS

ILIKUWA kazi rahisi kwake kupenya kwenye Bongo Fleva kutokana na sauti yake tamu kusikika kwenye ngoma ya ‘Uswazi Take Away’ ya Chegge.

Kwa sasa Malaika anatamba na singo yake ya Rarua. Ni  miongoni mwa wasanii wa kike wanaobamba watu wa rika zote, kiasi kwamba hata Rais Magufuli aliwahi kumtaja kama msanii anayemkubali miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva.

Katika mahojiano na Swaggaz, Malaika ambaye hivi karibu ametua nchini akitokea Marekani alipokuwa akifanya ziara yake ya kimuziki kwa takribani miezi sita, ameeleza kwa kina changamoto na mafanikio ya tour yake hiyo.

Anasema lengo kuu la ziara yake hiyo ilikuwa ni kukuza muziki wake, kuongeza wigo wa mashabiki na kuitangaza Tanzania na kwamba ameweza kufanya jumla ya shoo 17 nchini Marekani.

 

AMEJIFUNZA NINI?

“Mashabiki wa kule kiukweli wanamthamini msanii awapo jukwaani na kazi yake. Hawataki kuona unakosea… kazi kazi tu. Uzuri wanakuja watu wa mataifa mbalimbali kwahiyo unajitangaza zaidi.

“Nimejifunza mengi kupitia shoo zangu na hata shoo za wasanii wengine wa kule, maana nilipata nafasi ya kwenda kujiona live wakipafomu jukwaani.”

 

CHANGAMOTO

Anasema alikwenda Marekeni katika kipindi ambacho barafu huanguka hivyo ilimtia hofu sana kwamba anaweza asipate watu wa kuhudhuria kwenye shoo zake, lakini haikuwa hivyo.

“Hakuna msanii wa hapa Bongo aliyewahi kwenda Marekani kwenye shoo kipindi cha barafu, lakini mimi nilipata moyo ingawa nilikuwa na hofu kuwa inawezekana nisipate watu wengi lakini nashukuru hali haikuwa mbaya.

“Mwanzo ugumu ulikuwa kwenye kulitawala jukwaa kwa sababu hapa nyumbani nilizoea kupafomu kwenye  shuguli za Serikali lakini nilikuwa sijawahi kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye kama zile ambazo mara nyingi ni katika klabu na matamasha.

“Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuchukuliwa kwenda kuwaburudisha watu, nimejifunza na kupata ujuzi wa kutosha ambao kwa muda mrefu nilikuwa sijaupata ukilinganisha nilikuwa napiga shoo kwenye majukwaa makubwa,” anasema.

 

KOLABO SAFI

Mbali na shoo, Malaika anasema katika muda aliokuwa Marekani amefanya nyimbo nyingine zikiwamo kolabo na wasanii wa nchi mbalimbali ikiwamo Marekani, Nigeria na Sierra Leone.

“Nimefanya kazi nyingi na nzuri, ni suala la muda tu na kuchagua wimbo gani uanze kutoka. Mashabiki wangu wakae tayari, nitaanza kuziachia muda wowote, moja baada ya nyingine,” anasema.

 

KOLABO NA BIEBER

Kuhusu taarifa zilizosambaa kuwa Malaika ana mpango wa kufanya kolabo staa wa muziki wa Pop nchini Marekani, Justin Bieber, anasema ni kweli alikuwa na mpango lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na Bieber kubanwa na ratiba zake binafsi za kikazi.

“Kolabo na Bieber ni taarifa za kweli na mipango ilishafanyika. Nilipokuwa kwenye shoo California, nilikutana na uongozi wake, tukaongea jinsi ya kufanya kazi wakakubali lakini kwa bahati mbaya ratiba ilimbana kutokana na tour ndefu nje ya Marekani.

“Tumekubaliana kwamba tutafanya kazi atakapomaliza tour yake ya mwaka mmoja. Nilipokamilisha ziara yangu, nimerudi nyumbani nikiwasikilizia atakapokuwa tayari maana tumebadilishana mawasiliano,” anasema.

 

UNAIKUMBUKA ILE VIDEO YENYE VIHOJA?

Mwisho Malaika alizungumzia video aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Instagram siku chache baada ya kuanza ziara yake nchini marekani na kuwa gumzo kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Wengi walisema video hiyo ilikuwa kinyume na maadili yetu, huku wengine wakisema kuwa alikuwa anatafuta kiki.

“Tangu naanza kufanya sanaa sijawahi kufikiri kutumia kiki kukuza muziki kwahiyo haikuwa kwa ajili ya kiki bali niliposti kama video nyingine ambazo nilikuwa nikiziposti.

“Mimi ni binadamu, kwahiyo kuna wakati nafanya ninachojisikia, isitoshe ile video sijaona kama ina tatizo lolote na mimi ni msanii hivyo napaswa kufanya chochote kitakachowafurahisha mashabiki wangu.

“…nadhani labda ilionekana tofauti kwa sababu watu hawajawahi kuniona nikikata mauno kiasi kile. Lakini ukitazama kwa makini hakuna cha ajabu, maana wapo wasanii wengi tu huwa wanaposti video zaidi ya zile,” anasema Malaika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles