28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONTENA 262 YA MCHANGA WA DHAHABU YAKAMATWA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, akikagua makontena 262 yenye mchanga wa dhahabu, yaliyobainika katika bandari ya Dar es Salaam jana.

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imesema imebaini makontena mengine 262 yenye mchanga wa dhahabu, yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu ya MOFED (zamani ZAMCARGO) iliyopo Kurasini, Dar es Salaam.

Kubainika kwa makontena hayo, yaliyokuwa yakisubiri taratibu za kiforodha kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia kitengo cha makontena kinachoendeshwa na kampuni binafsi ya TICTS, kumekuja siku tatu tu baada ya Rais Dk. John Magufuli kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua makontena 20 yenye shehena ya mchanga wa madini kutoka migodi mbalimbali iliyopo Kanda ya Ziwa.     

Rais Magufuli alifika bandarini siku hiyo kukagua utekelezaji wa agizo lake la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wenye madini kutoka migodini.

Akizungumza baada ya kukamata makontena hayo, Mkurugenzi Mkuu wa  TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, alisema yalibainika jana  katika msako mkali unaoendeshwa na mamlaka hiyo.

“Makontena yote hayo yalikuwa na lakiri (seals) za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na yalikuwa yanashughulikiwa na kampuni ya usafirishaji wa mizigo ya Freight Forwarders Tanzania Limited iliyopo Dar es Salaam,” alisema Mhandisi Kakoko.

Alisema mbali na makontena hayo, TRA pia imegundua mengine sita yaliyokuwa yameshaingizwa bandarini tayari kwa kusafirishwa.

Aliongeza kuwa orodha ya makontena hayo  inaonyesha yalifika bandarini hapo kwa nyakati tofauti kutoka mgodi wa Buzwagi uliopo Kahama unaosimamiwa na Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia   na kontena nyingine zimetoka Pange Mines.

Alitoa wito kwa kampuni za madini zenye shehena za mchanga zijitokeze na kuonyesha mizigo waliyonayo   kabla haijabainika katika msako unaoendeshwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchi nzima.

Wakati Mkurugenzi huyo wa TPA akisema hayo, Mhandisi Asa Mwaipopo ambaye ni Meneja Mkuu-Uhusiano na Serikali wa Kampuni ya Acacia, alisema makontena hayo ni halali kwani yamekaguliwa na kulipiwa kodi zote kupitia mamlaka za Serikali.

“Tuna migodi miwili inayozalisha copper concentrate. Copper concentrate zinapakiwa kwenye makontena na kuyasafirisha nje, makontena hayo yanazalishwa kwa idadi kubwa, kwa siku  mgodi mmoja unazalisha kontena nne au tano. Kwa hiyo kwa siku ‘average’ ni kama kumi kwa migodi miwili.

“Yanasafirishwa kwa idadi ya makontena 25 au 30, labda kwa wiki mara moja au mbili hivi, kwa hiyo ni ‘production chain’ ambayo ipo kwa miaka mingi na hata sasa inaendelea kwa sababu uzalishaji unaendelea,” alisema.

Alisema lilipotokea katazo la Rais Magufuli Machi 2, mwaka huu la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa dhahabu, uzalishaji ulikuwa unaendelea kama kawaida.

“Ni kama vile ukisimamisha kiwanda cha bia ku-produce (kuzalisha) bia, kuna bia zitakuwa kwenye bottling (chupa), kuna bia zitakazokuwa kwenye packaging, it’s a chain. Kwa hiyo kuna makontena ambayo yalikuwa kwenye yadi ya clearing and forwarding, ni wakala wetu, kuna makontena ambayo yalikuwa yamepelekwa bandarini kwa ajili ya kuwa loaded (kupakiwa), kuna makontena yalikuwa barabarani,” alisema na kuongeza:

“Hayo makontena ndiyo idadi hiyo ambayo wamekwenda wameyakuta kwenye yadi ya mtu aliyekuwa anakaribia ku-export (kusafirisha nje), ni makontena halali yamepimwa, yamewekewa seal na TRA, yamewekewa seal na Tanzania Mineral Audit Agency, mamlaka za Serikali, yametolewa leseni ya export na Wizara ya Nishati na Madini, yana leseni yamelipiwa loyalty (mrabaha) asilimia nne na Serikali imechukua hizo hela,” alisema Mwaipopo.

Machi 2 mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishaji wa mchanga wa madini ya dhahabu nje ya nchi, akisema kuwa ni wizi kwa sababu mchanga ukifika huko unachambuliwa na kupatikana dhahabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles