25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MBOWE: JPM AKISHINDA 2020 NAJIUZULU SIASA

Na OSCAR ASSENGA, MUHEZA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Rais Dk. John Magufuli atakuwa kiongozi wa kwanza nchini kuvunja rekodi ya kutawala kwa kipindi cha miaka mitano badala ya 10 kama walivyofanya watangulizi wake.

Mbowe aliyasema hayo jana wakati akizindua tawi la wakereketwa wa chama hicho lililopo eneo la Mpakani, Kata ya Kwakifua, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Katika hoja hiyo, Mbowe alisema Rais Magufuli ataongoza kwa muhula mmoja kwa kuwa utawala wake hauthamini utu wa binadamu, na ikiwa vinginevyo, yuko tayari kuachana na siasa.

“Watu wa Tanga mmechelewa sana kuiondoa CCM madarakani, tulifanya makosa kumchagua Rais wa Awamu ya Tano, matokeo yake wote tunaisoma namba. Tunaanza maandalizi mapema, maana huyu rais atatawala miaka mitano na akiendelea naacha siasa,” alisema Mbowe.

Alisema tofauti na utawala huu, watangulizi wa kiongozi huyo walikuwa wakifanya kazi kwa waledi na kutenda haki huku wakisikiliza changamoto zilizowakabili wananchi.

“Taifa linapita kwenye wakati mgumu kutokana na utawala wa mabavu uliopo, ambao umechangia kuwepo manung’uniko makubwa kwa jamii ya Watanzania na kuwaacha wanyonge wakiwa hawana la kufanya.

“Utawala wa awamu ya tano umekuwa wa kibabe, usioheshimu utu, ubinadamu, jambo linalosababisha maisha magumu kwa Watanzania waliouamini,” alisema Mbowe.

Alisema kutokana na hali hiyo, chuki na manung’uniko miongoni mwa Watanzania ambao watafanya uamuzi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020, vimeongezeka.

“Ndugu zangu hakuna kipindi cha kujenga mageuzi kama hiki, kwa sababu utawala huu umejenga simanzi na manung’uniko kwa Watanzania wengi, ambao leo hii wanapata shida kwa hali halisi ya ugumu wa maisha na kuacha kuthamini utu wa watu.

“Walikuwa wanaamini wanaweza kuutesa upinzani hapa nchini, lakini badala yake mambo hayo yamejirudi ndani ya chama chao (CCM),” alisema Mbowe.

Alisema hivi sasa gharama za maisha kwa wananchi zimeongezeka na kipato kikipungua, huku Serikali ikiwa haina mpango wa kunusuru hali hiyo.

SUALA LA NAPE

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye aliondolewa na Rais Magufuli katika nafasi yake wiki hii, anakijua chama kuliko kiongozi huyo.

Alisema Nape ni miongoni wa watu wanaoijua CCM kwa muda mrefu na kufanikiwa kukijenga chama hicho kuliko ilivyo kwa Rais Magufuli.

Mbowe ambaye yuko katika ziara ya siku sita mkoani hapa, alisema kinachotokea hivi sasa ni nchi kuendeshwa kwa maamuzi ya mabavu ambayo yanalenga kuwatisha viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma na wananchi.

Alisema kila jambo lina taratibu za kisheria, hasa inapotokea mmoja kati ya viongozi walioteuliwa akijaribu kutenda haki baada ya kuminywa kwa demokrasia ya habari na uamuzi wake kuonekana hauna mashiko.

Mbowe alisema tafsiri hiyo inaonekana ni kupuuzwa kwa kiongozi huyo kwa madaraka aliyopewa.

“Utawala wetu una ubaguzi wa hali ya juu, yule kiongozi ambaye anaonekana kuwa mstari wa mbele kutetea umma, ndiye anaonekana hafai na kutumbuliwa, yule anayekwenda kinyume na taratibu za nchi, ndiye anaonekana mwema kwa mtawala. Hii ndiyo nchi yetu,” alisema Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles