Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuteua wakuu wa wilaya wapya 27 na wengine 19 kuondolewa, wadau mbalimbali wamejitokeza wakidai huo ni mkakati wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kutengeneza mazingira ya kuchakachua kura za maoni ili kiweze kushinda kwa urahisi.
Wadau hao pia wamedai katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kuteua viongozi hao waweze kutengeneza mikakati ya ushindi katika maeneo yao.
Hata hivyo, akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwashangaa wapinzani kwa kupinga uteuzi huo huku akisisitiza kuwa lingekuwa jambo la ajabu kama wanasiasa hao wangeupongeza.
“Ningeshangaa kama wanasiasa wangesifia uteuzi huo…kwa sababu ndiyo uwezo wao wa kufikiri uliopoishia, ninaomba Watanzania kuwasamehe bure,” alisema Nape kwa kifupi.
Wakizungumzia uteuzi huo mpya, baadhi ya wanasiasa akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, walisema hawaoni umuhimu wa nafasi hizo wakidai uteuzi huo umelenga kuandaa timu ya uchakachuaji wa kura katika uchaguzi mkuu na kura ya maoni ili kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Walidai uteuzi huo ni maandalizi ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu kwa sababu nafasi hizo hazina umuhimu kwa taifa na kwamba hatua hiyo inaongeza mzigo wa gharama kwa wananchi.
WASOMI
Baadhi ya wasomi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini waliuita uteuzi huo kuwa ni wa siasa na umelenga kuhakikisha Katiba mpya inapita.
“Uteuzi huo ni wa siasa zaidi kuhakikisha CCM inashinda kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha Iringa.
Profesa Mpangala pia alitoa tahadhari kwa mteule wa Kinondoni ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Paul Makonda, akisema kiongozi huyo ameteuliwa kimkakati ili kuhakikisha anasimamia upitishwaji wa Katiba mpya katika eneo lake.
“Uteuzi wa Paul Makonda umekuja kimkakati, lengo ni kuhakikisha Katiba Inayopendekezwa inapita kwenye kura za maoni si vinginevyo.
“Ndiyo maana Rais Kikwete amefanya mabadiliko hayo kwa sababu anajua kuwa kinachofuata ni uchaguzi mkuu, lazima aangalie watu watakaoweza kutetea maslahi ya chama chake,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, idadi kubwa ya waliochaguliwa wanafanya kazi kwa kufuata matakwa ya viongozi wao jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupata ushindi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Hajji Semboja, alisema nafasi ya ukuu wa wilaya ni ya siasa zaidi kwa vile haiangalii sifa ya mtu anayeteuliwa kushika nafasi hiyo.
“Hizi nafasi za U-DC na RC ni za wanasiasa zaidi ndiyo maana wanachaguliwa bila kuangalia sifa ya mtu… hali ambayo imesababisha kuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.
“Yaani kila nilipopita nasikia Makonda, Makonda…, nikajiuliza ni mtu wa aina gani? Kumbe wanamtuhumu kwenye tukio la Jaji Joseph Warioba, nikajiuliza kwanini aliteuliwa…ila nikapata jibu kwa sababu nafasi zenyewe zimetoka kisiasa zaidi,” alisema Profesa Semboja.
Alisema ili kupata viongozi bora, Serikali inapaswa kuwapa elimu ya uongozi ili wakichaguliwa waweze kujua wajibu kwa wananchi na jinsi ya kujiheshimu.
WANAHARAKATI
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema hakuna kificho, pangua pangua na uteuzi huo wa ma-DC wapya una sababu maalumu.
Alisema ni wazi wakuu hao wa wilaya wamechaguliwa kwa ajili ya kwenda kushughulikia uchaguzi mkuu ujao utakaofanyia Oktoba, mwaka huu.
Sioni sababu hasa iliyomfanya rais apangue wakuu wa wilaya katika kipindi hiki ambacho tumebakiza miezi minane tufanye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Dk. Bisimba.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA, Irene Kiria, alisema hatua hiyo ni gharama ambayo inahitaji fedha wakati katika huduma nyingine za jamii Serikali imekuwa ikisema haina fedha.
“Gharama zinakuja kwa kuwa ma-DC hao watahitaji kuhamishwa kwa wale waliohamishiwa vituo vipya na wale wapya pia wana mahitaji yao zaidi.
“Kupangua wakuu hao ni kupoteza fedha za umma bure wakati kuna sekta zinazohitaji fedha kwa ajili ya mahitaji muhimu.
“Hili suala la wakuu wa wilaya tumeshalizungumza mara nyingi, hata kwenye rasimu ya pili ya Katiba iliyosimamiwa na Jaji Joseph Warioba ilitaka watu hao wasiwepo, lakini tunandelea kuona fedha zinatumika kwa ajili yao bila sababu ya msingi,” alisema.
MNYIKA
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema kuhamishwa vituo kwa wakuu wengi wa wilaya miezi michache kabla ya kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ni mkakati wa wakuu hao ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenda kupiga kampeni za ndiyo kwa Katiba haramu.
“Wakuu wote ni wajumbe wa kamati za siasa za CCM, hivyo huu ni mkakati kwenda kupiga kampeni za ndiyo kwa Katiba haramu iliyopitishwa kiharamia katika Bunge Maalumu na baadaye kuhujumu upinzani kuelekea uchaguzi mkuu kuliko ufanisi wa utendaji wa Serikali,” alisema Mnyika.
Akizungumzia uteuzi wa aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi katika mikoa kadhaa, Zelothe Steven, alisema utachochea wakuu wengine wa polisi kuhujumu upinzani.
“Uteuzi wa Zelothe utaendelea kuchochea wakuu wengine wa polisi kuhujumu upinzani katika kipindi cha utumishi wao kwa kujipendekeza kwa rais ambaye pia ni amiri jeshi mkuu ili wakistaafu utumishi wao waendelee kupata fadhila kupitia nafasi kama za ukuu wa wilaya,” alisema Mnyika.