23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda azua taharuki

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

LEONARD MANG’OHA NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KAULI mbalimbali zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa ziara zake zimezua taharuki jijini humo.

Kwa nyakati mbalimbali wakati wa ziara zake,  Makonda anadaiwa kutoa kauli za vitisho hasa kwa watumishi wa umma.

Kutokana na hali hiyo, Chama cha ACT-Wazalendo kimemshtaki mkuu huyo wa mkoa katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Utawala Bora ili imuwajibishe.

Katika taarifa yake iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Katibu wa Ngome ya Wanawake wa chama hicho, Esther Kyamba alisema kauli alizozitoa Makonda zimewadhalilisha watumishi hao.

“Tumesikitishwa na kuhuzunishwa na kauli zisizo za kiuongozi na zisizozingatia kanuni za maadili ya utumishi wa umma zinazoendelea kutolewa na RC Makonda.

“Jana (juzi), katika mkutano anaouita wa kutatua kero kwa wakazi wa Dar es Salaam aliendelea kushindwa kutatua kero na badala yake kuongeza kero ya kudhihaki, kudhalilisha kukejeli na kutukana hadharani wananchi anaowaongoza na watumishi anaowasimamia kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya Watanzania,” alisema.

Kyamba alisema kitendo cha Makonda kumtolea lugha ya udhalilishaji Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni, Rehema Mwinuka akiwa Mabwepande kwa kumtamkia kwamba “Hawa ndio vichaa tunaohangaika nao, toka hapa”. Hakikubaliki.

“Kauli hiyo imetushtua sana,tunalaani kwa nguvu zetu zote, kauli kama hii si tu haikupaswa kutolewa na kiongozi mkubwa katika ngazi ya mkoa lakini pia ni kauli mbaya ambayo ililenga kumdhalilisha Rehema na kumvunjia heshima yake mbele ya umma,” alisisitiza.

Alisema kutokana na udhalilishaji huo uliofanywa na Makonda, wameshawasilisha mashtaka yao dhidi yake mbele ya Tume, wakiitaka imwajibishe kwa kitendo chake hicho cha utovu wa nidhamu na maadili ya utumishi wa umma.

“Ngome inamtaka mkuu huyo wa mkoa kutambua kuwa kwa kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma, kanuni ya 65(1) inamtaka mtumishi wa umma, “kuepuka kufanya vitendo viovu au kutamka maneno yanayolenga kuwaaibisha watumishi wa ngazi moja, za chini yao au wa vyeo vya juu,” alisema.

Alisema kitendo alichofanya, kumwaibisha na kumtolea lugha ya udhalilishaji, Mwinuka ni kinyume cha Sheria na Kanuni za Utendaji katika Utumishi wa Umma.

“Tunaitaka Tume ifanye uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya matamshi mbalimbali yaliyotolewa na Makonda ambayo yalikiuka sheria ya Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma.

“Tunayataka mashirika na asasi mbalimbali zinazosimamia haki za binadamu, haki za jinsia na utawala bora kupaza sauti dhidi ya kauli isiyo ya kiuongozi ya  Makonda, Ngome na Chama kwa ujumla tutaendelea kuwasemea wanyonge wote popote walipo kwa kadri ya uwezo wetu,” alisema.

Hata hivyo, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imebariki kauli za vitisho dhidi ya watumishi wa umma, ambazo zimekuwa zikitolewa na mkuu huyo wa mkoa wakati wa ziara zake.

Akizungumza na MTANZANIA jana Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa sekretarieti hiyo, Joseph Ishengoma, alisema kuwa kauli hizo zimekuwa na lengo la kuwabana watumishi wasiotekeleza majukumu yao ili kutatua kero zinazowakabili wananchi.

“Kama lengo ni kupunguza kero zinazowakabili wananchi ni lazima atumie lugha ya ukali pale ambapo mambo hayaendi vizuri na watumishi hawawajibiki kutatua kero hizo.

“Lakini katika kutoa kauli au maagizo anaweza kutumia lugha ambayo watu wataitafsiri tofauti kutokana na ‘temple’ aliyokuwanayo wakati anatoa kauli hiyo, wakati mwingine kauli inaweza kutolewa kulingana na uzito wa kile kinachozungumziwa” alisema Ishengoma.

Aliongeza kuwa mkuu wa mkoa ana mamlaka ya kumwajibisha mtumishi wa umma ambaye yupo katika eneo lake la kiutawala kwa kumwagiza mkurugenzi ambaye atafanya hivyo kwa kuzingatia kanuni na sheria inavyoelekeza mtumishi kuchukuliwa hatua.

Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kutoa matamko yanayoonekana kuvunja sheria.

Agosti 26, mwaka huu, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) , Bahame Nyanduga alimwandikia barua ya kumtaka Mkuu huyo wa mkoa kufika katika ofisi za makao makuu ya Tume hiyo kujieleza kwa kile Tume ilichokiona kuwa ni kejeli kwa Tume pamoja na jumuiya yote ya watetezi wa haki za binadamu.

Tume hiyo iliona kuwa maagizo aliyoyatoa Mkuu huyo wa Mkoa kwa Jeshi la Polisi wakati wa kuaga miili ya askari Polisi watatu waliouawa Mbande, mkoani Dar es Salaam. hayana msingi wa kisheria na hayako ndani ya mamlaka ya Mkuu wa Mkoa.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1)(f) na (i) pia Kifungu cha 27(1) na (2) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura Na. 391 ya Sheria za Tanzania 2002, THBUB ina mamlaka ya kuchunguza mwenendo wa mtu au taasisi yoyote kuhusiana na utendaji wa kazi zake zinapokiuka mipaka ya madaraka yake, ili kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji huo.

 

Katika mkutano huo Makonda alisema “Askari ukikutana na mtu yoyote kwenye msitu wewe piga alafu hao haki za … za binadamu basi nataka haki za askari wangu kwanza”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles