Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Paul Makonda, amesema umeme bado ni changamoto inayowatesa wananchi na kuwataka watendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kujitathimini.
Hayo ameyasema leo Desemba 21, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari akitoa taarifa ya mambo mbalimbali yanayohusu CCM.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni mvumilivu, hadi ukiona anafikia kufanya mabadiliko na kuvunja bodi ujue maana yake jambo hilo halivumiliki.
“Swali letu kama chama nawauliza Tanesco, kweli mnapokaa na hizi kelele au maumivu ya watanzania juu ya kukatika kwa umeme, nyinyi mnajisikia fahari? Na kama mnajisikia fahari mnajiona kweli mnastahili kumuwakilisha Rais Dk. Samia?
“Zipo sababu zinakulikana lakini zipo nyingine ni uzembe.Unaona mtendaji yeye yupo ofisini nasaini tu na kutoa maelekezo, nenda ‘site’ kaoneshe tatizo wananchi waone lakini unapokaa ofisini unatengeneza mtazamo tofauti. amesema Makonda.
Amesema kuanzia mwakani 2024, CCM haitamuonea huruma wala haya mtu mzembe na rushwa.
Kuhusu migogoro ya ardhi
Katibu huyo amesema wamedhamiria kumaliza changamoto ya maji na migogoro ya ardhi nchini kutokana na Wizara ya Ardhi kuanzisha kliniki za ardhi.
Ameeleza kuwa moja ya mikoa iliyokuwa na migogoro ya ardhi ni Dodoma na walielekeza wizara kupambana kuhakikisha wananchi ondoa changamoto hiyo na hadi sasa zaidi ya wananchi 40,000 wa mkoa huo wamepatiwa hati.
Amesema kliniki hiyo inaendelea nchi nzima lengo kuhakikisha migogoro hiyo inamalizika nchini ambapo tayari zaidi ya hadi 5000 za kidigitali zimetolewa.
Awataka wananchi kutoka maoni
Katika hatua nyingine Makonda amewetaka wananchi kutoa maoni ya juu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050 ili kuweza kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Aidha amewetaka watu walioanza kujipitisha majimboni na kwenye Kata kutaka ubunge na udiwani kuacha mara moja kwani bado wanawatambua viongozi waliopo madarakani kwa sasa.
“Watu waache kujipitisha pitisha, waache chokochoko hizo ili wawape nafasi wabunge na madiwani wafanye kazi kwani muda wa kampeni bado haujafika,” ameeleza.
Ametangaza kuanza ziara ya pili katika mikoa 10, ikiwamo Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Simiyu na Pwani na kuwataka watendaji wa sehemu hizo hujiandaa na wananchi kujipanga kutoa kero zao.