Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameunda kamati ya watu 17 itakayopambana na biashara za ngono, madanguro na ushoga katika mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makonda alisema kamati hiyo itajumuisha wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi.
Alisema wengine katika kamati hiyo ni kutoka Bodi ya Filamu na Madaktari na wataalamu wa saikolojia.
“Kamati hiyo itashughulikia watu wanaofanya vitendo vya ushoga, wanaotengeneza filamu za ngono ambako tayari kuna nyumba 24 inadaiwa kufanya hivyo, watu wanaofanya biashara za ngono katika mitandao ya jamii,” alisema Makonda.
Alisema kamati hiyo itakuwa inafanya shughuli zake makao makuu yake Mburahati na inatarajiwa kuanza kazi rasmi Novemba 5, mwaka huu.
“Kuna watu wameamua kujitangaza na kufanya biashara kupitia mitandao kama James Delicious, Anti Milk, Dida Mtamu, Bariki, Abbas na kundi la WhatsApp la Pachupachu kamati hii itakwenda kushughulikia,” alisema Makonda.
Alisema kufanya ngono kinyume cha maumbile ni kinyume cha sheria namba 124 hivyo wataadhibiwa kwa kuvunja sheria hii.
Alisema kamati hiyo pia itawashughukia wanaotapeli kwa njia za mitandao na kwa kutumia majina ya viongozi.
Licha ya hali hiyo alisema ana taarifa kuhusu kuwapo baadhi ya vituo vya ‘massage’ kutumika kama madanguro ya kufanyia ngono.
“Niwaombe kuwa mapambano haya si ya serikali ni ya Watanzania wote, tushikamane kwa kuwa maadili ya mwafrika si haya ndiyo maana tukiomba hayafanikiwi ni kutokana na mambo ambayo hayakubaliki katika imani zote,” alisema Makonda.
Aliwaomba watetezi wa haki za binadamu kuacha kutetea tabia hizo kwa kuwa kwa sheria za Tanzania ni kinyume cha sheria kwa sababu imeweka bayana.
“Ndugu zangu wa haki za binadamu na nchi zilizopokea ushoga mtambue kuwa Tanzania tuna sheria zetu ni kosa la jinai,” alisema Makonda.