AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amefanya ziara kukagua athari za mafuriko katika Wilaya ya Kinondoni.
Alisema serikali imeanza kukarabati miundombinu iliyoathiriwa na mvua inayoendelea kunyesha yakiwamo madaraja, barabara, mito na mifereji.
Akizungumza jana baada ya kutembelea nyumba zilizoathiriwa na mvua hiyo eneo la Jangwani, Makonda alisema miongoni mwa maeneo yanayoboreshwa ni eneo la Mto Msimbazi wenye urefu wa kilometa 19 na eneo la Jangwani ambalo maboresho yake yatagharimu zaidi ya Sh bilioni 200 ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Alisema hadi sasa watu wawili wamefariki dunia kutokana na mvua.
Pia aliwapa pole wananchi waliokumbwa na mafuriko wakiwamo wale ambao mali zao zimeharibiwa na wengine kulazimika kuyahama makazi yao.