NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, amekana kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.
Amedai kwamba alichozungumza kiliungwa mkono na viongozi wa juu wa chama hicho akiwamo John Malecela na Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya.
Makonda alidai hayo jana katika majibu yake aliyowasilisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa.
Katika majibu hayo, Makonda anadai taarifa aliyotoa kwa waandishi wa habari iliungwa mkono na Malecela mjini Dodoma, na Msuya alipotakiwa kutoa maoni yake na waandishi wa habari mjini Moshi pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula akiwa jijini Mbeya na Rais Jakaya Kikwete.
“Rais hakuishia kuunga mkono hoja hiyo bali alielekeza chama kuchukua hatua dhidi ya wote ambao wanatuhumiwa kufanya kampeni kabla ya muda.
“Si kweli kwamba maneno niliyotoa yalikuwa yanawakashifu walalamikaji na kuwaathiri hadi kuwasababishia madhara,” alidai.
Makonda anadai kwamba walalamikaji walitakiwa kufuata katiba, kanuni na taratibu zilizowekwa ndani ya chama kwa kuwasilisha malalamiko hayo ndani ya chama badala ya kukimbilia mahakamani.
Mdaiwa huyo mwishoni aliiomba mahakama kuyatupa madai yaliyopo dhidi yake kwa gharama.
Mahakama iliwapa nafasi walalamikaji kuwasilisha hoja za nyongeza kama zipo Mei 5, mwaka huu na kesi hiyo itatajwa Mei 11, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Msindai na Guninita wanaiomba mahakama hiyo imwamuru Makonda awaombe msamaha na kuwalipa kila mmoja Sh milioni 100.
Msindai na Guninita wanaotetewa na Wakili Benjamini Mwakagamba, wanaiomba mahakama pamoja na mambo mengine itoe zuio la kudumu kwa Makonda asizungumze tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Pia wanaomba Makonda kulipa riba pamoja na gharama za kesi na nafuu nyingine.
Makonda anadaiwa kuwa katika mkutano wake alitoa maneno na kudai kuwa Msindai na Guninita ni vibaraka wanaotumiwa kuharibu chama cha CCM kwa nguvu ya pesa.
Wadai hao walidai kuwa maneno hayo yaliyotolewa na Makonda yamewafanya waonekane ni viongozi ambao hawafai kuongoza CCM.