Na Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhi Sh milioni 34.5 Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa upasuaji wa moyo watoto wanaotoka familia masikini.
Fedha hizo zilitolewa na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond akishirikiana na wasanii wenzake ili kuunga mkono juhudi za Makonda.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makonda aliwashukuru watu wote ambao wamejitokeza kuunga mkono juhudi zake kuhakikisha watoto wanapata huduma.
“Siku ya kwanza nilisema nitawasaidia watoto 60, sio kwamba nilikuwa na fedha, ila nilisema kiimani, kuna tofauti kati ya kuwa na nazo na imani, imani niliyokuwepo nayo ni kwamba Mungu ana uwezo wa kufungua milango kuwaleta watu ambao wanaweza kunisaidia ili niweze kutimiza ahadi ambayo niliiahidi.
“Japo nilienda kuomba watu wanisaidie, pia nilimwomba Mungu madaktari wa hapa aendelee kuwatia moyo, nawashukuru kwa kazi na huduma nzuri mnayoendelea kufanya, hatimaye watoto wote waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na hawajapata shida yoyote.
“Namshukuru Diamond na timu yake, nilivyoenda kwenye kipindi nilimwambia nina watoto ninaowalea kama wewe, tofauti yenu wana matatizo ya moyo, muziki umekuwa sehemu ya kurejesha furaha ya watoto hawa,” alisema Makonda.
Aliwashukuru wasanii wengine kama Irene Uwoya, Juma Jux na Mboso ambao wote walichangia watoto wawili, wakati RayVann na Queen Darleen walichangia mtoto mmoja mmoja na kufikisha watoto 45 watakaofanyiwa upasuaji.
“Naendelea kupokea michango kupitia kamati ya kusaidia watoto inayoongozwa na Charles Kimei, makampuni mkipata barua kutoka kwa mwenyekiti wangu mtupe ushirikiano ili kusaidia kuokoa maisha ya watoto wenye uhitaji,” alisisitiza Makonda.
Diamond alisema yupo tayari kuwasaidia watoto wenye uhitaji wa kufanyiwa upasuaji wa moyo na ataendelea kutoa ushirikianao bila kuitwa.
“Nimpongeze Profesa Janabi kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuwa anafanya kwa moyo wote, watoto wanaumwa, kiukweli nimepita wodini kuna sehemu nimeshindwa kuingia jinsi watoto wanavyoumwa.
“Kama wasanii, mashabiki na wanaotusapoti kazi zetu ni wazazi wa watoto wenye matatizo ya moyo, nitoe wito kwa Watanzania kwa yeyote mwenye uwezo wa kusaidia kidogo alichonacho kusaidia ili kurudisha furaha ya watoto walioko hospitali,” alisema Diamond.
Mkurugenzi wa Taasisi ya JKCI, Profesa Mohamed Janabi aliwashukuru wasanii na Makonda na watu wote waliojitolea kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo, kwani watoto wengi waliosaidiwa hali zao zimeimarika na wengine wanaendelea na maisha yao ya kawaida.
“Katika kila watoto 100 wanaozaliwa, mmoja lazima awe na ugonjwa wa moyo, wengine hawana uwezo wa matibabu, nawashukuru wote wanaojitokeza kuwasaidia watoto hawa,” alishukuru Profesa Janabi.