27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONDA AIBUKA, AONYA WAKURUGENZI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, jana aliibuka kimya kimya katika uzinduzi wa barabara mpya ya Shimo la Udongo Kurasini Wilaya ya Temeke, baada ya kutoonekana hadharani kwa zaidi ya wiki moja.

Katika muda wote huo nafasi ya Makonda ilikuwa inashikiliwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva ambaye alimwakilisha Makonda wakati akimpokea Rais Dk. John Magufuli akitokea ziara ya mikoa ya kusini.

Lyaviva pia alimwakilisha Makonda katika kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita moja iliyogharimu zaidi ya Sh milioni 350 imejengwa na Kampuni ya wazalendo ya Grand Tech Tanzania Limited kwa kiwango cha zege inaungana na ile ya Kilwa inayotokea katikati ya jiji.

Katika uzinduzi huo, Makonda aliahidi  kushirikiana na wakandarasi wazawa huku akitishia kuwashughulikia wakurugenzi wa halmashauri za jiji watakaoingia mikataba mibovu na wakandarasi.

Kwa upande wake, Meneja Operesheni wa Kampuni ya Grand Tech Tanzania, Masito Mwasingo aliipongeza Serikali ya Mkoa wa Dar es salaam kwa kuwaamini na kuwapa fursa ya kuonyesha ujuzi wao.

 

VITA DAWA ZA KULEVYA

Februari 2, mwaka huu Makonda alitaja kwa mara ya kwanza majina ya baadhi ya wasanii, akiwamo Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu na askari polisi aliodai wanahusika na dawa za kulevya.

Siku sita baadaye, alitaja majina mengine 65 ya watu maarufu akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephati Gwajima pamoja na mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji akiwataka wafike Kituo  Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kuhojiwa juu ya tuhuma hizo.

Februari 14, mwaka huu  Makonda alikabidhi majina mengine 97 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya kwa Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga na kuahidi kutoyatangaza hadharani kabla ya kuyafanyia uchunguzi.

Wakati jana ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu sakata hilo liibuke na kuibua hoja kinzani katika jamii, taasisi mbalimbali zikiwamo za kiserikali na ndani ya Bunge.

Suala la elimu ya Makonda ni miongoni mwa mambo ambayo yameonekana kuteka kwa kiasi kikubwa mijadala ya sasa na hata kujenga hisia za kuchepusha ama kubadili upepo wa vita hiyo ya dawa za kulevya.

Chimbuko la elimu ya Makonda limeibuliwa na Askofu Gwajima kuzungumza jambo hilo hadharani.

Hatua hiyo ya Askofu Gwajima ilitafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kijamii kuwa ni hatua yake ya kulipiza kisasi baada ya kutajwa katika orodha ya dawa za kulevya.

Hata hivyo si Makonda wala mamlaka nyingine ambayo imepata kulizungumza kwa undani suala hilo, zaidi yeye mwenyewe kupuuza taarifa hizo kila anapoulizwa na vyombo vya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles