28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Wadau washauri elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ipewe nguvu

Na Damian Masyenene

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini Tanzania 2015/16-2019/20 iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy  Mwalimu, kwa wadau na watoa huduma za afya jijini Dodoma Agosti 19, mwaka huu, Serikali imevuka lengo la asilimia 80 ililojiwekea katika Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto (2016-2020).

Aidha, kuimarishwa kwa ubora wa huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto kumeleta ongezeko kubwa la akinamama wanaohudhuria mara nne au zaidi kwenye kliniki ya wajawazito kutoka akinamama 747,524 (asilimia 39) mpaka akinamama 1,758,191(asilimia 81) Juni 2020.

Katika hilo, idadi ya wanawake wanaotumia huduma za afya ya uzazi kabla ya ujauzito na baada ya kujifungua imeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2015/16 hadi asilimia 43 mwaka 2020, huku kiwango cha wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kikiongezeka kutoka akinamama 1,226,707 (asilimia 64) mwaka 2015 mpaka akinamama 1,801,603 (asilimia 83) Juni mwaka huu.

“Kwa kutumia takwimu za mfumo wa kufuatilia vifo vitokanavyo na uzazi, tumeshuhudia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa zaidi ya asilimia 71 ukilinganisha na vifo vilivyotolewa taarifa kupitia utafiti mwaka 2015/2016 (TDHS).

“Hali hii inaashiria kuwa tutakapofanya utafiti wa hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini ifikapo mwaka 2021, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi nchini Tanzania kitakuwa kuwa chini ya vifo 190 kwa vizazi hai 100,000 ukilinganisha na vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 kama ilivyotolewa taarifa kwenye utafiti wa mwaka 2015/16,” alinukuliwa Waziri Ummy.

Mkurugenzi wa Shirika la Thubutu Africa Initiative, Jonathan Manyama

Licha ya jitihada hizo za serikali katika kuimarisha afya ya uzazi na mtoto, changamoto zimeendelea kuwepo, huku elimu ya afya ya uzazi hususan uzazi wa mpango ikitajwa kutolewa kwa kiwango kidogo miongoni mwa vijana, hali ambayo inaendelea kushuhudia vijana wakikumbwa na matatizo ya kupata mimba zisizotarajiwa, kupata mimba wakati bado wananyonyesha, kushindwa kumudu familia na kuziteleza pamoja na kuendelea kuambukizwa magonjwa ya zinaa.

Kutokana na hali hiyo, Mtanzania Digital imefanya mahojiano na baadhi ya vijana na wadau mbalimbali wa afya hususan afya ya uzazi mkoani Shinyanga ambao wametoa maoni na kushauri juu ya elimu ya afya ya uzazi kwa vijana izidi kupewa msisitizo kwani huwasaidia vijana kujitambua, kufanya maamuzi na kuwa na kizazi salama na chenye afya.

Wadau hao wameeleza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwani vijana wana nafasi kubwa ya kubadilisha jamii, ambapo wakipanga maisha yao itawasaidia kuhimili yajayo, kwani wengi wanashtukizana na kushindwa kuhimili matokeo hali ambayo hupelekea changamoto ya utoaji mimba, hivyo elimu hiyo itasaidia kupata akina mama wenye afya njema wakatakaolipatia taifa kizazi chenye afya njema.

Mratibu wa shughuli za kijamii shirika la Doctors With Africa, Gasaya Msira

Mmoja wa wadau hao, Jonathan Manyama ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Thubutu Africa Initiative, amesema afya ya uzazi kwa vijana ni sehemu ya eneo wanalolifanyia kazi kwa sababu vijana ndiyo kundi kubwa katika jamii yetu kuanzia ngazi ya taifa hadi vijiji, kwahiyo ndiyo injini ya maendeleo na shughuli nyingi za maendeleo zinawagusa.

Amesisitiza kuwa manufaa ya afya ya uzazi humsaidia kijana kulinda afya yake, kuwa na familia bora, kuwa na watoto wenye afya njema na malezi bora, ili kijana afanikishe hayo inabidi awe na taarifa ya afya ya uzazi itakayomsaidia kufanya maamuzi.

“Kupitia mradi wa USAID Tulonge Afya tuna jukwaa la Naweza ambalo tunafanya kazi na makundi ya vijana, mfano kuna vijana wa kike wamezalishwa wako kwa wazazi wao ukifuatilia unagundua alikuwa hajajipanga na hakupata taarifa sahihi……Tuna vikundi vya hao mabinti kuwafundisha kuhusu mambo mbalimbali ya afya ya uzazi na namna ya kujikinga na mimba, magonjwa ya zinaa, kujitambua na kuwa na nguvu ya kusema hapana wanapokuwa hawajawa tayari kwa ajili ya ngono.

“Tunafanya hivyo ili mabinti hawa watakapoamua kupata mtoto mwingine wawe tayari kwa kipindi wakitakacho, Pia tunacho kipengele cha uzazi wa mpango, waweze kupanga muda wa kupata watoto, siyo unakuta mtoto ana miezi sita tu tayari wanapata mimba nyingine.

“Tunawaelimisha vijana wa kiume kuhusu matumizi ya kinga (kondomu) kwa sababu wanazo changamoto nyingi wanapokutana na wanawake wakubwa (majimama) wanalelewa kwahiyo ili wawaridhishe wanafanya mapenzi bila kutumia kinga, wengine hutoboa kinga na kutovaa kabisa,” ameeleza Manyama.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa vifaa/zana za afya ya uzazi, amesema kuwa kama wadau wanashiriki kupaza sauti kwa mamlaka kuhakikisha nyenzo za uzazi wa mpango zinapatikana kwa ajili ya makundi yenye uhitaji, pia kuongeza uhitaji kwa kuhamasisha watu kwenda hospitali kupata huduma hizo.

Kwa upande wake, Gasaya Msira ambaye ni Mratibu wa shughuli za Kijamii katika Shirika la Doctors With Africa (CUAMM), amesema vijana kwa ujumla wakipata elimu ya afya ya uzazi kwa usahihi na kuitekeleza kwa vitendo ina manufaa mengi, kwani itawasaidia kuwa na familia zilizo bora wanazoweza kuzimudu na kujipa nafasi nzuri ya kutimiza malengo yao.

“Ukipanga familia unaweza kuwa na familia mbayo inafuata ushauri wa kitaalam mfano muda wa kunyonyesha na kuwa na mpango wa umri wa watoto unaoweza kuwahudumi kielimu, kijamii, makuzi na makazi bora. Vijana wakiyaishi maisha hayo na wao wakawa mabalozi wanasaidia kuibadilisha jamii na kuwaelimisha marafiki wanaowazunguka.

“Vijana wakipata elimu hiyo, mfano kwa mama anapata manufaa makubwa, kwani uzazi wa mpango humpumzisha mama na kumsaidia mtoto kunyonya kwa muda unaoshauriwa kitaalam, kwa sababu kwenda bila mipango wakati mwingine humkatisha mtoto kunyonya kutokana na mimba kuingia bila mipango,” amesisitiza.

Mmoja wa vijana, Dorice Nestory ambaye ni mama wa mtoto mmoja, anasema aliamua kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango kutokana na hofu baada ya mkasa uliompata rafiki yake ambaye alipata ujauzito akiwa na miezi sita tu baada ya kujifungua, hivyo aliamua kwenda hospitali kupata huduma za afya ya uzazi ili asipate ujauzito ambao haujapangwa na apate nafasi ya kumnyonyesha mtoto wake kwa muda sahihi.

Naye Gracious Mashaka ambaye ana mtoto wa miezi mitatu, anasema aliamua kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango kabla hajaanza kukutana na mmewe kutokana na kuepuka kupata ujauzito wakati bado ana mtoto mchanga, huku akibainisha kuwa wanawake wengi wanaohudhuria kliniki hawapati elimu ya kutosha kuhusu afya ya uzazi hususan uzazi wa mpango, na kujikuta wakibahatisha ama kupata mimba wakati bado wananyonyesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles