Na Yohana Shida, Geita
Nchini Tanzania Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la Kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo sensa ya mwisho kufanyika ilikuwa mwaka 2012.
Sensa ya mwaka 2022 iliyofanyika kuanzia Agosti 23, inakuwa ni ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini, kuchapisha na kusambaza takwimu za Kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.
Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.
Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji.
Manufaa ya Sensa katika Huduma ya Afya ya Uzazi
Akifanya mahojiano maalumu na Mtanzania Digital, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk. Japhet Simeo anakiri takwimu za sensa ya watu kwamba zinamanufaa makubwa katika kuboresha huduma ya afya ya uzazi na huduma ya mama na mtoto.
Dk. Simeo anasema sensa ya watu na makazi inagusa moja kwa moja sekta ya afya, hususan afya ya uzazi na huduma ya mama na mtoto kwa kuwa inasidia kupatikana taarifa za watu ambao wapo kwenye umri wa kupata ujauzito (Reproductive Age).
“Hii kwa kujua idadi yake kwanza inaisaidia Serikali kuweka mikakati na mipango kwa ajili ya kulilea hili kundi, kwa ajili ya afya bora na huduma sawia za afya ya uzazi.
“Jambo la pili serikali inajua idadi ya watu na wategemezi kwa kaya (Family Size) na kwa kuhusianisha na uchumi wa familia inatambua uwezo wa familia wa kuhimili matokeo yatokanayo na afya ya uzazi kwa mwanamke.
“Uwezo wa familia hulingana na kipato na idadi ya familia na hali halisi ya wanakaya inakupa taswira kubwa tatu ya kwanza uwezo wa kaya kuhudumia mwanamke yeyote anayepata changamoto za ujauzito katika ile kaya.
“Cha pili usalama wa chakula kwa maana ya masuala ya lishe kutokana na ukubwa ile familia, na jambo la tatu ni kutambua uwezo wa kugharamia masuala ya afya na rufaa za ndani katika jamii kutoka eneo moja hadi eneo jingine,” anafafa Dk. Simeo.
Anaeleza, pia sensa inaisaidia serikali kujua idadi ya watoto ambao wana anuani halisi katika kaya na idadi za watoto wasio na anuani halisi (Watoto wa mtaani) na pengine kung’amua uhalisia na ongezeko la watoto hao na kuchukua hatua mbadala.
“Kwa mlengo huo inatupa picha kwamba kundi hili (watoto wa mitaani) jinsi gani tuweze kulifikia mapema kabla halijajihusisha na masuala ambayo yanaweza yakawafanya wakapata watoto wakiwa na umri mdogo hususani watoto wa kike.
“Kwa hiyo serikali inaweza ikatambua kundi hili na ikaweka mikakati mapema na madhubuti kwa ajili ya kuweza kuwakinga wasiingie katika mazingira hatarishi kama ngono zisizo salama na pengine wakapata mimba zisizotarajiwa,” amesema.
Dk. Simeo anabainisha eneo jingine muhimu la mageuzi ya huduma za afya ya uzazi kupitia sensa ni katika uboreshaji wa mindombinu ya eneo la afya ya uzazi na mtoto.
“Tunaona kwamba serikali inakuwa na uwezo wa kutambua ni maeneo gani na kwa idadi gani ya wakazi wake wana uhakika wa kupata huduma za afya na kwa kiwango gani.
“Tukihusisha afya ya uzazi na mtoto, tunagundua kwamba kupitia sensa, inakuwa ni rahisi kubaini sehemu kubwa yenye wakazi wengi, lakini pia wenye kiwango cha juu cha kuzaliana (Fertility Rate),” amesema Dk. Simeo.
Dk. Simeo anasema kupitia kuhusianisha idadi ya watu na kiwango cha miundombinu iliyopo itakuwa ni rahisi kupeleka miundombinu ya ziada ili kuweka usawia wa huduma na idadi na kupunguza umbali wa kina mama kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya ya uzazi.
Anasema kabla ya kufikia maboresho ya miundombinu serikali itakuwa imeng’amua takwimu za makundi maalumu na uwezo wao wa kiuchumi na kufanikisha mgawanyo sahihi wa miundombinu na vifaa tiba kulenga kupunguza vifo viyokanavyo na uzazi.
“Tukumbuke makundi haya yenye uwezo mdogo wa kiuchumi ndio makundi yanayoathirika zaidi na tabia za ngono zembe, na wanapopata ujauzito hawapati huduma zilizo bora na baadhi yao wanaweza wakapoteza watoto ama wao wakafariki, ama wote kwa pamoja.
“Hii pia inasaidia serikali kupitia upya mikakati ya kuhamasisha matumizi ya uzazi wa mpango, hasa kwa kupitia yale maswali na majibu tuliyopata kwenye sensa ya watu, itatupa fursa ya kubuni upya ama kuboresha mikakati tuliyonayo kuongeza uzazi wa mpango.
“Pia itatusaidia kujua uwiano wa kila mtumishi wa afya anahudumia watanzania wangapi, na serikali itaweza kutafuta njia mbadala, kwani imeshaanza kwamba kama eneo lina makusanyo makubwa halmashauri inaweza ikawa na mpango wa kutoa ajira za muda kwenye sekta ya afya,” amesema Dk. Simeo.
Dk. Simeo anahitimishi kuwa, iwapo kutakuwa na ushiriki madhubuti na wananchi kutoa takwimu sahihi katika sensa ya watu na makazi, serikali itaweza kugawanya kwa uwiano mzuri miundombinu, watumishi na vifaa tiba katika sekta ya afya na kuboresha huduma ya afya ya uzazi.
Mwenendo wa Huduma ya Afya ya Uzazi Nchini
Akisoma Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu anasema huduma za afya zimeimarika ndani ya mwaka mmoja katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi, 2022.
Waziri Ummy anasema kwa kipindi hicho vituo vya kutolea huduma za afya nchini vilivyosajiliwa vimeongezeka kufikia 8,549 ikilinganishwa na vituo 8,458 mwaka 2020. Kati ya hivyo, Hospitali ni 404, Vituo vya Afya 956 na Zahanati 7,189
Anasema hayo ni matokeo ya serikali kuendelea kuwekeza ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya ya Uzazi, ikiwa ni pamoja huduma kabla ya kujifungua, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
“Serikali imeendelea kutoa elimu ya umuhimu wa akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022, wajawazito 1,398,778 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya sawa na asilimia 79.5.
“Kulingana na takwimu zinazokusanywa kutoka katika vituo vya kutolea huduma zinaonesha kuwa vifo vya Watoto vimeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma ya afya ya uzazi.
“Vifo vya Watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 8,190 mwaka 2020 hadi vifo 6,741 mwaka 2021. Vifo vya Watoto wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 2,657 mwaka 2020 hadi vifo 1,092 mwaka 2021,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy anabainisha pia kiwango cha vifo vya Watoto umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 3,482 mwaka 2020 hadi vifo 1,512 mwaka 2021 ambapo takwimu hizi hazijumuishi vifo vinavyotokea kwenye ngazi ya jamii.
Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23
Waziri Ummy anabainisha kwa mwaka 2022/23, Wizara imepanga kutumia kiasi cha Sh bilioni 554.2 kwa ajili ya Matumizi ya kawaida sawa na asilimia 50 ya bajeti tengwa, ambapo kiasi cha sh. bilioni 331.5 ni kwa ajili ya mishahara ya Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Anasema pia kiasi cha sh bilioni 222.7 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo huku wizara inakadiria kutumia sh. 555.1 bilioni 32.05 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 50 ya bajeti tengwa.
Anaeleza kati ya hizo, fedha za ndani ni sh. bilioni 410.29 na fedha za nje ni Sh bilioni 144.8 na kufanya jumla ya bajeti ya Wizara kuwa Sh trillioni 1.109 ili Wizara kutekeleza malengo iliyojiwekea kuboresha huduma za afya ikiwemo Huduma ya Afya ya Uzazi.