28.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Ufahamu wa njia asilia ya uzazi wa mpango

Na Yohana Paul, Mwanza

UZAZI wa Mpango kwa njia asilia maana yake ni mbinu zile za kuzuia mimba isipatikane katika tendo la ndoa ambazo zinafuata maumbile, pasipo kuhusisha vifaa wala kemikali, bali hutegemea ufahamu wa uwezo wa mwanamke kupata au kutopata mimba wakati wa kufanya tendo la ndoa.

Ufahamu huo unahusisha kufanya tendo la ndoa pasipo kufanikisha uchavushaji na urutubishwaji wa mayai ya mwanamke  ingawa wanawake wanaonyonyesha na wanapenda kukwepa mimba wanaweza kufanya tendo la ndoa kwa kutegemea kukatizwa kwa hedhi wakati wa kunyonyesha.

Mbali ya ufahamu huo wa jumla, uzazi unaweza kupangwa kwa kutofanya tendo la ndoa siku 13 hivi ambapo katika mzunguko wa hedhi kuna uwezekano wa kupata mimba na kinyume chake wanandoa wanaweza kulenga uzazi kwa hakika zaidi wakifanya tendo la ndoa kwa kutumia vizuri siku zinazouwezesha.

Ukiachana na kupanga uzazi kwa njia ya ufahamu pasio matumizi ya njia za kisasa, vilevile wanandoa ama wachumba wanaweza kutumia ufahamu huo kuchagua jinsia ya mtoto mtarajiwa kwa kufanya tendo la ndoa siku ambapo kwa kawaida mbegu ya jinsia hiyo ndiyo inayowahi kuungana na kijiyai katika tumbo la uzazi.

Ufahamu wa njia ya asili ya uzazi wa mpango hutegemea pia mbinu za uelewa wa kalenda, kwa hufuatilia mzunguko wa hedhi na kwa kuzingatia urefu wake ambapo huwezesha kutambua mwanamke anapoweza kupata mimba na asipoweza kupata mimba.

Sifa za Uzazi wa Mpango wa Njia Asilia 

Uzazi wa mpango kwa njia asilia una sifa bainifu kadhaa ikiwemo uwezekano wa kutumika kudhibiti afya ya uzazi, kwa kuwa mabadiliko katika mzunguko wa hedhi na kusaidia kumtahadharisha mtumiaji kuhusu kujitokeza kwa matatizo ya kike.

Aidha njia za asilia zinaweza kutumiwa na wanawake wote katika kipindi chote cha uzazi, bila kujali kama anakaribia kumaliza kuzaa, ananyonyesha, au anapata mzunguko wa hedhi usio wa kawaida kwa sababu nyingine.

Pia njia hii imeweza kusadia kuongeza ufahamu wa jinsi mwili wa mwanamke unavyofanya kazi, na unamwezesha kudhibiti zaidi uzazi wake mwenyewe pasipo kuwa mtegemezi zaidi kwa wengine na hivyo kutambua mwenendo wa mzunguko wa hedhi.

Njia hii ya upangaji uzazi mbali  na changamoto zilizopo imebainika kutokuwa na madhara yoyote ya kiafya kwa wale wanaoielewa, tofauti na ilivyobainika kwa baadhi ya njia za kisasa na mbinu nyingine.

Kwa mtazamo mwingine pia njia hii kama itaweza kueleweka kwa usahihi zaidi itasaidia kuondoa gharama zisizokiwa za lazima ikilinganishwa na mbinu nyingine.

Tofauti na mbinu mbalimbali ambazo zina athari za muda mrefu, ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unawezesha kubadili mara moja kutoka uamuzi wa kuzuia mimba isiyotamaniwa hadi ule wa kuilenga mimba inayotamaniwa.

Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutumika pia kwa lengo la kupata mimba ya jinsia inayotamaniwa zaidi iwapo tu mke na mme wataweza kuelewa sahihi mzunguko wa hedhi wa mke.

Dalili za msingi za Kushika Mimba

Zipo mbinu kadhaa ambazo hutegemea mabadiliko yanayoashiria uwezekano wa kutunga mimba kwa mwanamke kwa kufuatilia mzunguko wote wa hedhi na  kubaini wakati ambapo inawezekana kushika mimba ama kutokushika mimba.

Kwa mjibu wa tafiti zilizofanyika zimebainisha dalili tatu za msingi za uwezekano wa kushika mimba kwa mwanamke ambazo ni jotomsingi la mwili, ute wa uke na mkao wa mlango wa kizazi.

Aidha wanawake wengine wanaweza kung’amua pia dalili nyingine za ziada kulingana na mzunguko wa hedhi, kama vile maumivu na uzito tumboni, maumivu mgongoni, ulaini wa matiti na maumivu ya kudondosha kijiyai.

Kwa njia nyingine inawezekana pia kufanya uchunguzi wa mkojo kwa kutumia vifaa vya kubashiri udondoshwaji wa kijiyai, na uchunguzi wa ute au ugiligili wa seviksi kwa kutumia hadubini.

Isitoshe, ipo njia ya kufuatilia uwezo wa kushika mimba kwa tarakilishi ambapo inapotumika kwa usahihi, na kuendana na mafundisho endelevu, baadhi ya tafiti zimeonyesha mbinu fulani za namna hiyo kuwa na asilimia 99 za ufanisi.

Kupanga Ujauzito wenye jinsia

Tafiti zinaeleza kuwa mke na mme wanaweza kuchagua mtoto wa kiume au wa kike kwa 85% ya hakika wakifanya tendo la ndoa kwa kupanga kulingana na ute wa uke kuwa wa kuvutika na kuteleza au siyo.

Tafiti za kibaiolojia zinaelekeza kwamba jinsia ya mimba itakayotungwa ama mtoto atakayezaliwa inategemea tu kromosomu za mbegu za baba ambazo ni nusunusu: X kwa kuzaa watoto wa kike na Y kwa kuzaa watoto wa kiume.

Aidha utafiti umebainisha kuwa mbegu zenye kromosomu X ni dhaifu kidogo nazo huogelea polepole, lakini zinaishi muda mrefu. Kumbe zenye kromosomu Y zina nguvu zaidi na kuogelea upesi, lakini hufa upesi.

Kupanga jinsia ya Kiume

Kwa kuzingatia tabia hizo mbili tofauti, maharusi wakitaka mtoto wa kiume wanatakiwa kufanya tendo la ndoa siku ya kwanza baada ya kilele (kujisikia kuteleza) na kuendelea kwa miandamo 6 ya hedhi. 

Ambapo Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miandamo 6, waanze kuonana siku ya kilele na siku inayofuata na  iwapo mwanamke amekosa siku ya kilele, yaani kama utelezi wa ute unaendelea siku inayofuata, waonane tena siku inayofuata.

Kwa njia hiyo mbegu zenye kromosomu Y tu zitafikia kijiyai kilichochopoka, kwa sababu mbegu zenye kromosomu X zinaogelea polepole tu na hivyo kupata uhakika wa kiwango kikubwa kupata mtoto wa kiume.

Kupanga  jinsia ya kike

Kinyume chake, iwapo mme na mke wakitaka mtoto wa kike wanatakiwa kufanya tendo la ndoa siku ya kwanza ya ute wa uzazi na baadaye wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele na waendelee hivyo kwa miandamo michache.

Watalaamu wanaeleza kaama mwanamke hajapata mimba baada ya miezi michache, wafanye tendo la ndoa siku ya kwanza na ya pili ya ute wa uzazi halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele na waendeleehivyo kwa miandamo michache. 

Aidha, tafiti zinaelekeza kama mwanamke hajapata mimba baada ya miezi michache, wafanye tendo la ndoa pia siku ya tatu ya ute wa uzazi halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache.

Kwa njia hiyo mbegu zenye kromosomu Y zitakufa kabla ya kuweza kuungana na kijiyai, na hivyo zitabaki zenye kromosomu X kuwa na nafasi hiyo, na hivho siku nzuri ya kupata mtoto wa kike ni kufanya tendo la ndoa siku mbili kabla ya kilele cha utelezi.

Kumbuka

Kwa kiwango fulani mbinu ya kalenda hukumbwa  na ufaisi hafifu kutokana na ukweli kwamba mbinu hii hutegemea dalili, hasa kwa baadhi ya wanawake na ya vipindi vya maisha yao kutokana na uwepo wa mabadiliko ya mzunguko wa hedhi inayoweza kusababishwa na hali ya hewa, magonjwa na mfumo wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles