Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
MASKINI ni neno pana ambalo kila mtu anaweza kulitafsiri kwa namna anayona na kutokana na kipato chake ama cha jamii inayomzunguka.
Pia kwa nchi, kuna namna mbalimbali za kupima umaskini na kuugawanya katika makundi mbalimbali ambapo kwa Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inajukumu la kukusanya takmwimu mbalimbali ikiwamo za umaskini wa kaya na mtu mmojammoja.
Ni kupitia takwimu hizo, Taasisi kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), hutambua kaya maskini na kuziingiza katika mradi wa kuwapa fedha kulingana na idadi ya wategemezi katika kaya ili kuweza kuzikwamua.
Pamoja na takwimu za NBS, kaya masikini zinazoingia kwenye miradi ya Tasaf, pia hutambuliwa kwa njia jumuishi kupitia mika mikutano ambayo hufanywa kwenye ngazi za mitaana huku pia watendaji wa mitaa wakihusika katika zoezi hilo.
Licha ya kiasi kidogo ambacho hutolewa kwa walengwa huku kikiwa na matumizi makubwa, baadhi ya kaya zinakiri kwamba sasa zinaweza kutoka matika mradi huo na kuachia wengine wenye shida zaidi kunufaika.
Hadija Kaaya (42) ni mkazi wa Mtaa wa Rerili, Kata ya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, anasema awali alikuwa anafanya biashara ndogo ambayo ilikuwa bado haimpi uhakika wa milo mitatu kwa siku.
Anasema alipoanza kupata fedha za Tasaf, alikuza mtaji wake hadi na baadaye alianza kukopa kwenye taasisi ndogo za fedha na kukuza zaidi mtaji wake.
Anasema kwa sasa ana biashara mbalimbali ikiwamo mama lishe, genge na kibanda cha kuunza vinywaji vya baridi na vile vyenye kileo.
Anasema pia kupitia Tasaf, mtoto wake aliweza kupata mkopo wa kwa asilimia 100 ambapo kwasasa anaendelea na masomo ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Kwasasa kweli nikiambiwa nipishe wenye shida zaidi yangu wala sintosita,” anasema Hadija.
Kwa upande wake Blandina Massawe (46), mkazi wa mtaa wa Magereza, anasema yeye alipoanza kupewa fedha hizo alianza kuwekeza kwenye miradi ya kufuga kuku na mbuzi.
Anasema baadaye aliuza sehemu ya mifugo hiyo na kuanza kununua ulezi ambao aliutumia kwa kutengeneza kimeoa ambacho hutengeneza pombe aina ya mbege iliyo mashuhuri katika mkoa wa Kilimanjaro.
Anasema alianza na gunia moja na sasa mtaji wake umeongezeka na kufika magunia matatu.
“Mimi natengeneza kimea kisha nauzia ambao wanatengeneza pombe, biashara yangu inaendelea kukua na sasa nafikiria kuanza biashara ya kuku wa nyama,”anasema
Anasema ili afikie kwenye biashara yake, yuko mbioni kumalizia nyumba yake ambayo itakuwa pia na eneo kubwa la kufugia tofauti na anapoishi sasa ambapo amepangisha.
“Mambo mengi nashirikiana na mume wangu ambaye yeye ni mkulima, Tasaf ilivyonifikisha sasa naweza kutoka nikaachia wengine,”anasema.
Moja ya changamoto zinazowapata wanufaika wa Tasaf akiwamo Massawe na wengine wengi, ni namna ya kupata mikopo nafuu zaidi ya kukuza biashara zao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe, anasema asili ya watu wa Moshi ni wachapa kazi ambao wanajituma kuachana na umaskini.
Anasema kaya masikini ambazo zimetambuliwa kwenye manispaa hiyo ni 1,227 ambazo zina wastani wa watu wane.
Gembe anasema kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri ambayo hutengwa kwaajili ya kusaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wanawake ambao wamekuza mitaji yao na wapo tayari kukopeshwa wanaweza kujiunga na kupata fedha hizo.
Anasema kwa uzoefu wake, wanawake wamekuwa moja ya kundi linalorejesha vyema mikopo hiyo ya halmashauri ambayo haina riba.
“Kwasasa kuna vikundi vitatu vyenye watu watano kila kimoja na kuanzia mwakani mapema watapata hii mikopo,”anasema.