26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Makala| PPRA ilivyopiga hatua miaka mitatu ya Dk. Samia

*Ni katika eneo la Usimamizi katika manunuzi ya umma

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Machi 19, mwaka huu Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inatimiza miaka mitatu tangu alipoingia madarakani Machi 19, mwaka 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli.

Tumeshuhudia mabadiliko mengi yaliyofanyika katika kipindi hiki. Sekta ya Ununuzi wa Umma haikuwachwa nyuma, nayo pia ina mengi yanayoweza kuelezewa kama mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi mahiri wa Rais Samia.

Mapinduzi hayo yamepelekea uwepo wa matokeo chanya kwa wadau wa sekta hiyo na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mkurugenzi Mkuu, Eliakim Maswi anasema wameshuhudia mafanikio makubwa kutokana na kazi za usimamizi wa shughuli za Ununuzi wa Umma ambazo wamezitekeleza katika kipindi hiki cha miaka mitatu.

Kuanzishwa kwa Mfumo Mpya wa Ununuzi kwa njia ya Kielektroniki (NeST)

Kabla ya kuingia madarakani Serikali ya awamu ya sita, ununuzi ulifanyika kwa kutumia mfumo wa TANePS.

Mfumo huu uligubikwa na changamoto nyingi zilizopelekea wadau wa sekta kulalamika na kushindwa kuutumia kwa ufasaha katika michakato ya ununuzi.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Umma(PPRA) wakiwa kwenye kikao cha Mamlaka hiyo kilichofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.

Hali hiyo iliilazimu Serikali ya Awamu ya Sita kufikiria kwa upya namna ya kuboresha Sekta ya Ununuzi ili kuweza kukidhi matakwa ya wadau nchini na nje ya nchi.

Mnamo Julai 2022, ujenzi wa mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki ujulikanao kama NeST ulianza rasmi kujengwa. Jumla ya moduli sita ziliainishwa na kuwekwa katika mpango wa ujenzi ili kuhakikisha michakato yote ya ununuzi inafanyika kidigitali.

Mpaka kufikia Julai 2023 tayari moduli mbili muhimu, moduli ya usajili e-registration na moduli ya michakato ya unununuzi e-tendering zilikamilika ujenzi wake.

Kukamilika kwa moduli hizi mbili kubwa ilikuwa ni moja ya mafanikio makubwa sana katika ujenzi wa mfumo wa NeST hivyo mpaka kufikia Oktoba 1, 2023 Taasisi zote nunuzi zilianza rasmi kutumia Mfumo wa NeST.

Kufuatia waraka uliotolewa na Mlipaji Mkuu wa Serikali Taasisi zote nunuzi zilielekezwa kuhakikisha zinaanza kuutumia kikamilifu mfumo wa NeST na ndipo mfumo wa TANePS ulipozimwa rasmi.

Mpaka sasa tayari moduli nyingine kubwa ya mikataba imekamilika na itaanza kutumika hivi karibuni.

Mfumo wa NeST imeondoa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wadau wa ununuzi wa umma zikiwemo vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili ambapo hapo awali ilikuwa ni tatizo kubwa.

Maswi anasema miongoni mwa mabadiliko na mafanikio yaliyoshuhudiwa kwenye mfumo huu ni kuwa umeongeza matumizi ya tekinolojia katika ununuzi wa umma, pia mfumo umerahisisha michakato katika ununuzi wa umma kwa kuongeza uwazi na usawa katika ununuzi na kupunguza muda wa urasimu katika michakato ya ununuzi.

Hii inaenda sambamba na kuongeza ushindani kwa wazabuni kushiriki katika ununuzi wa umma,kupunguza gharama za michakato ya zabuni za umma kuongeza ufanisi na kupata thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa umma.

“Hadi kufikia Februari, 2024 jumla ya tuzo za mikataba zenye thamani ya Sh 1,954,269,683.55 zimetolewa kwa makundi maalum kupitia zabuni za umma zilizotangazwa na taasisi za umma kupitia mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (NeST), ambapo kundi la vijana wamepata tuzo za mikataba zenye thamani ya Shilingi 709,162,838.00, wanawake 1,166,769,845.55 na Wazee 78,337,000.00,” anaeleza

Kujenga uwezo na kutoa ushauri

Moja ya jukumu la PPRA kisheria ni kujenga uwezo kwa wadau na kutoa huduma za ushauri kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo ununuzi wa Umma.

Akielezea jinsi Mamlaka ilivyofanikiwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Maswi anasema katika juhudi za kujenga uwezo na kutoa ushauri kwa taasisi nunuzi, PPRA imeendesha mafunzo maalum kuhusu sheria ya ununuzi wa Umma, ambapo kati ya Aprili, 2021 na Machi, 2024, imefanya mafunzo maalum (Tailor made training) kwa awamu kwa Taasisi za umma 83 na Halmashauri 50 na kuhudhuriwa na jumla ya washiriki 1,814.

Washiriki hao ni kutoka Taasisi za umma ambao wamejengewa uwezo kwenye sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali ya ununuzi wa umma, wakiwemo wakaguzi wa ndani, wakuu wa vitengo vya usimamizi wa ununuzi, wajumbe wa bodi za zabuni na Idara tumizi.

Vilevile, kati ya Aprili, 2021 na Machi, 2024, mamlaka imeendesha mafunzo ya pamoja 15 yanayohusu sheria, mikataba na zana za kutekelezea ununuzi, ambapo kati ya hayo, mafunzo 12 yalihudhuriwa na watumishi wa umma 1,291 kutoka taasisi nunuzi 381, huku mengine yakitolewa kwa wazabuni na kuhudhuriwa na washiriki 41, huku mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu yakifanyika mara mbili na kuhudhuriwa na washiriki 357.

Kufuatia kukamilika kwa mfumo wa NeST Mamlaka imetoa mafunzo maalum ya mfumo mpya wa ununuzi wa Umma wa kielektoniki (NeST) kwa Mikoa ikiwemo Sekretaieti za Mikoa na Halmashauri zote nchini. Jumla ya washiriki 1,687 kutoka katika Taasisi zipatazo 210 walipatiwa mafunzo hayo.

Aidha, Wakurugenzi 161 wa Halmashauri wamefanyiwa mafunzo ya NeST ili kuhakikisha kwamba halmashauri zote zinatumia mfumo kwa ufanisi ambapo ilisaidia kuongeza watumiaji wa mfumo katika halmshauri.

Hata hivyo, Mamlaka imefanikiwa kuwajengea uwezo makundi maalumu kwa nyakati tofauti jumla ya washiriki 928, wakiwemo wanawake 270 na watu wenye mahitaji maalum 158 na vijana 500 jijini Dodoma wamejengewa uwezo.

Tafiti zilizofanywa na Mamlaka

Kati ya mafanikio makubwa ya Mamlaka ni pamoja na uboreshaji wa kitengo cha utafiti ambacho kwa muda mrefu kilikuwa kimya bila kusikika. Katika kipindi hiki kitengo hicho kimeweza kufanya utafiti mkubwa na kujibu suala lililokuwa likisumbua vichwa vya watu kuhusu Force Account.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma(PPRA) Eliakim Maswi akiwa kwenye kikao cha Mamlaka hiyo ( baadhi ya wafanyakazi hawapo pichani) kilichofanyika hivi karibuni jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya( TUGHE) ngazi ya mkoa.

“Mamlaka imefanikiwa kufanya utafiti huo wa matumizi ya Force account ili kufanikisha upatikanaji wa thamani ya fedha (Value for money). Katika kuhakikisha kitengo hicho kinakuwa Madhubuti Mamlaka imekamilisha uandaaji wa sera ya tafiti na agenda ili kuainisha maeneo muhimu ya kufanya utafiti katika ununuzi wa umma na inatarajia kukamilisha tafiti mbili kabla ya mwaka kuisha,” anasema.

Uokoaji wa fedha za Serikali

Uwepo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma nchini umelenga kuisaidia serikali katika matumizi ya fedha zake katika ununuzi, kuhakikisha Thamani ya Fedha katika Ununuzi inaonekana.

Hivyo kutokana na lengo hilo, Mamlaka imepewa jukumu la kufanya kaguzi mbalimbali katika taasisi zote nunuzi.

Kwa mewaka wa fedha 2021/2022 hadi 2022/2023 matokeo ya kaguzi hizo inaonesha Mamlaka imefanikiwa kuokoa takriban Sh Bilioni 16.27 ambazo zilikuwa zinapotea katika michakato ya ununuzi. Fedha zilizookolewa zimeweza kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Tunamatarajio ya kuokoa kiasi kikubwa zaidi cha fedha kutokana na matumizi ya mfumo wa NeST,” Maswi alieleza .

Akielezea kuhusu fedha zilizotengwa katika ununuzi wa Umma, Maswi alisema zaidi ya Sh Trioni 25 imewekwa kwenye mfumo wa NeST kwa ajili ya kufanya ununuzi wa bidhaa,huduma na kazi za ujenzi,huku hadi kufikia machi 13,2024 mikataba ya zaidi ya Sh trilioni 2.7 imetolewa kwa wazabuni kupitia mfumo wa NeST, ambapo wazabuni 16,821 wamejisajili kwenye mfumo huo,’’ amesema Maswi.

Hivi ndivyo PPRA imekuwa ikitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Serikali iliyopo madarakani ya kupeleka huduma kwa wananchi na kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo, kama inavyoonyesha katika Sura ya kwanza ,Kipengele cha 8(e) ya Ilani hiyo wakati sura hiyohiyo kipengele cha 8 (f) ikielezea kujikita katika kutengeneza ajira zisizopungua millioni 8 katika sekta rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya vijana na hiki ndicho kinachoendelea kufanywa na PPRA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles