Na Nora Damian
Takwimu za Elimu (BEST) za mwaka 2020 zinaonyesha Mkoa wa Dar es Salaam una wanafunzi wenye ulemavu 345 ambao wako katika shule za Serikali na zisizo za Serikali.
Hivi sasa watoto wote bila kujali hali zao za kiafya na kimaumbile wanachanganywa pamoja ili kuondoa unyanyapaa na ubaguzi kwa watoto wenye ulemavu ambao wengi waliachwa nyuma kwa sababu ya imani potofu.
Hatua hiyo ni matokeo ya kuwapo kwa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2017 ukilenga kuondoa ubaguzi na kuwawezesha wanafunzi wote kupata elimu bora bila kujali hali zao za kiafya na kimaumbile.
Tangu kuanza kutekelezwa kwa mkakati huo kwa kiasi kikubwa kumekuwepo na matokeo chanya hasa kuhusu mtazamo uliokuwa umejengeka miongoni mwa jamii kuhusu watu wenye ulemavu.
Baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo hasi kwa kudhani kwamba watu wenye ulemavu hawana uwezo lakini sera ya elimu jumuishi imeleta majawabu juu ya dhana hiyo potofu.
Mathalani katika Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam watoto wenye ulemavu wameonyesha uwezo mkubwa.
Katika shule hiyo wanafunzi sita wasioona ndio wanaoshika namba za mwanzo kwenye darasa la saba.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Christina Wambura, anasema shule hiyo yenye wanafunzi 133 wenye mahitaji maalumu wengi wanafanya vizuri zaidi hasa wasioona.
“Kwa mfano darasa la saba wako watoto sita ambao hawaoni na katika namba za mwanzo ndio wanaoshika, jamii ielewe kwamba kila mmoja anayo haki ya kupata elimu. Shule zipo, wataalamu wapo, watoto wanaweza na wanafanya vizuri,” anasema Mwalimu Wambura.
Anasema pia watoto hao wanahitaji kupendwa, kuthaminiwa na kwamba wakisimamiwa wanafanya vizuri zaidi kitaaluma.
JITIHADA ZA MKOA
Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea kujizatiti kuimarisha sera ya elimu jumuishi kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki kwa watoto wenye ulemavu ili waweze kusoma bila vikwazo.
Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid, anasema wanaendelea kuielimisha jamii kuacha dhana potofu kuhusu watu wenye ulemavu kwani binadamu wote ni sawa.
“Ulemavu kama huna leo wewe ni mlemavu mtarajiwa kwahiyo ni binadamu kama wengine, mtu mwenye ulemavu wa viungo haina maana kwamba hana akili.
“Zamani mfano watoto wasioona, viziwi walikuwa na shule zao maalumu lakini sasa wanasoma ndani ya shule za kawaida hata mtoto mwenye ulemavu wa viungo au uoni hafifu anakuwa katika shule ya kawaida ile ndiyo elimu jumuishi,” anasema Maulid.
Aidha anasema licha ya kwamba walimu wanaendelea kuzalishwa katika Chuo cha Ualimu Patandi na vyuo vingine lakini wanayo mikakati ya kuwajengea uwezo walimu wa kawaida wabobee kwenye elimu maalumu.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Bonyokwa, Regina Ng’ongolo, anasema wanapogundua kuna watoto wenye ulemavu tunahakikisha tunawatambua waweze kupata haki zao.
“Kuna mashirika mbalimbali yanatoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi wakiwemo wenye ulemavu, kuna vikundi mbalimbali vya wanawake ambao nao wanaguswa kusaidia watoto.
“Kuna mtoto mmoja mwenye ulemavu baada ya kutambuliwa kupitia serikali ya mtaa kikundi kimoja kilijitolea kikampa baiskeli (kiti mwendo). Alikuwa akibebwa na mama yake mgongoni lakini sasa hivi ana baiskeli ambayo inamsaidia kupelekwa sehemu,” anasema Ng’ongolo.
MIUNDOMBINU RAFIKI
Miundombinu isiyo rafiki kwenye shule nyingi za msingi ni mojawapo ya vikwazo vinavyokabili utekelezaji wa sera ya elimu jumuishi.
Shule ya Awali na Msingi Ebonite iliyopo Manispaa ya Ubungo Mkoa wa Dar es Saalam, imeweka miundombinu rafiki kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kusoma bila vikwazo kama inavyoelekeza Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010.
Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Elimu Ebonite inayomiliki shule hiyo Thaddeus Njuu, anasema wanazingatia maelekezo ya Serikali kwa kuweka miundombinu rafiki ili kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kusoma bila vikwazo.
“Tunawajali wanafunzi wote bila kuwabagua, shule yetu ina majengo ya ghorofa ambayo mtoto anaweza kwenda kwa kutumia kiti mwendo hadi ghorofa ya tatu,” anasema Njuu.
Taasisi hiyo pia ina mpango wa kuanza kutoa mafunzo ya elimu maalumu ili kusaidia kukabili changamoto ya uhaba wa walimu hao
Makamu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Ebonite, Mwalimu Lusajo Mwaigusya, anasema wanataka kumjengea mwalimu tarajali maarifa na stadi kumwezesha kukabiliana na mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji wa mwanafunzi mwenye ulemavu atakayedahiliwa katika elimu ya msingi.