26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Miundombinu inavyoweka rehani elimu ya watoto Bukoba

*Mmiliki wa mtumbwi asipoamua hawaendi shule

*Wanatumia saa 4 kufika shuleni

Na Renatha Kipaka, Bukoba

Baadhi ya wananchi waishio katika kisiwa cha Msira ambacho ni kata ya mitaa mitano inayounda kata ya miembeni katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameomba Serikali kuwapatia shule kutokana na wanafunzi wanaoishi katika eneo hilo kushindwa kufika shuleni kwa wakati na wakati mwingine kuwa watoro kwa sababu ya kukosa usafiri wa uhakika.

Akizungumza na Mtanzania Digital jana mmoja wa wananchi hao, Mwajuma Kiwawa ambaye ni mama wa watoto watano amesema kukosekana kwa usafiri wa uhakika wa kuwezesha watoto wao kufika na kurudi shule kunawasababishia hofu ya usalama kwa watoto wao.

“Katika hili serikali itukumbuke maana usalama wa watoto wetu ni mdogo, kuna wakati watoto wanakwenda kusubiria usafiri kuanzia asubuhi hadi saa nne na wakati mwingine unakosekana kabisa hivyo wanakosa haki yao ya msingi ya kupata elimu,” amesema Kiwawa.

Upande wake Mwenyuekiti wa mtaa wa Msira, Yacoob Freish amesema tatizo hilo linekuwa sugu.

“Tatizo la usafiri kwa watoto wetu lakini pia lina sura tatu ambazo zinaweza kuwafanya kuishia njiani kimasomo, kwanza inaweza kuwafanya wanafunzi hawa kuwa wadumavu kielimu, pili usalama wao unakuwa mdogo sana kulingana na muda wanaporejea kutoka shuleni na tatu wazazi wao wana hofu sana juu yao, sababu hawaoni kama wanapata elimu stahiki pindi wanapokwenda shule sababu ya kuchelewa kufika.

“Ili kuondoa shida hii jamii ya msira tulijikusanya tukajenga darasa moja, malengo yetu yakiwa liwasaidie watoto wa awali angalau kujua kusoma na kuandika, lakini hatujawahi kupata walimu tangu tumetengeneza miundombinu hiyo, hivyo tunaomba serikali itusaidie kwani nimejaribu kwenda ngazi ya kata kuomba msaada bila mafanikio,” amesema Mwenyekiti huyo.

Richard Gaspar ni Diwani wa kata ya Miembeni ambaye anasema kuwa katika eneo hilo inasikitisha sana inapokuwa ni nyakati za mvua kwani watoto hao huwa wanashindwa kufika shule ikiwamo kunyeshewa na mvua hatua inayoharibu hata vifaa vyao vya kujifunzia kutokana na adha ya usafiri.

Ikumbukwe kuwa wanafunzi hao husafiri kwa kutumia boti ndogo ambayo ni mali ya mtu binafsi na pindi inapotokea siku kuna upepe mkali au mvu basi siku hiyo shule kuna kuwa hakuendeki.

“Jamani ule usafiri ni wa mtu binafsi, kuna siku anastisha safari, hivyo inakuwa imepita lakini mfano hawa watoto wakike wanakaa kwenye mwaroni wakisubiri usafiri hadi saa mbili usiku, usalama wao uko wapi na tunajaribu kutengeneza jamii gani, niombe wahusika katika hili wachuke hatua za maksudi kabisa.

“Nimekuwa nikifatilia kuona muda unaofikisha shuleni ni saa 4 hadi saa 5 hii inakuwa changamoto maana anayesoma darasa la kwanza anakuta vipindi vimekwisha na kwa wiki wanahudhuria siku mbili tu kitu ambacho ni hatari kwa mstakabali wa elimu kwao,” anasema Diwani huyo.

Mmiliki wa boti inayofanya safari zake kati ya Msira na Nyamkazi Lydia Mbeikya maarufu (Kesho mshara) amekiri kwa kusema kuwa boti yake inawabeba wanafunzi hao pale tu inapopata safari ya kwenda huko.

Anasema inakuwa ni changamoto kwani pindi abiria wanapokosekana siku hiyo basi safari inaharibika, kwa wanafunzi hao siku hiyo wanakuwa hawawezi kwenda shule.

“Mimi ninacho kiona ili kuwasaidia watoto wetu itapendaza kama ingejengwa shule huku ili kuondoa usumbufu unaowakabili wanafunzi hao maana wanakosa masomo, hivyo wanapishana na elimu,” amesema Lyidia.

Amesema kutoka Msira kwenda Nyamkazi inachukua dadika 30 na nauli Sh 2,000 kwa bei elekezi ila wanafunzi hawalipii usafiri .

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Hamid Njovu amesema wanafunzi wanaotoka Msira kuja katika shule ya msingi Nyamkazi ni 12 pekee.

Hivyo Njovu amesema kuwa Manispaa hiyo inafikiria kuwa na uwezekano wa kuweka shule shikizi au kuwapeleka watoto hao katika shule maalum za Mgeza viziwi ili waweze kukaa bweni.

“Niseme tu kuwa Manispaa ya Bukoba imejipanga kuwachukuwa watoto wote wanaosoma Nyamkazi ambao wanatokea Msira kwa kuwaweka bweni ili kuwafanya waendelee kupata haki za msingi kielimu, hivyo tushirikiane wote ili kuleta maendeleo yao,” amesema Njovu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles