29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Jinsi ya kumsaidia mtoto kupenda kula vyakula vyenye afya

Na Samwel Mwanga, Simiyu

MARA  Kwa mara wazazi na walezi wengi  hapa nchini wamekuwa wakihangaika kuwashawishi watoto wadogo kula vyakula vinavyousadia mwili kuwa na afya nzuri kama vile mboga ambavyo wengi wao huwa hawazitaki.

Ulaji wa vyakula visivyousaidia mwili kiafya mara nyingi huwafamnya watoto wanaoishi maeneo hasa ya mijini kunenepa mwili kupita kiasi na wengine hata kupata maradhi kama vile moyo na kisukari.

Kwenye maeneo mengi ya mjini hasa makao makuu ya Mikoa na Wilaya  kuna idadi kubwa ya watoto wenye matatizo ya afya yanayotokana na uzito wa kupita kiasi, lakini bado maeneo mengi hawajafanikiwa kuwasaidia watoto kula vyakula vyenye afya.

Mtaalamu wa masuala ya lishe katika kiwanda cha Unga wa viazi lishe katika Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aurelia Merikiory anasema ni vizuri kuweka mkakati wa kukabiliana na unene wa mwili kupita kiasi.

Anasema mkakati huo ulenge zaidi katika shule za chekechea na shule zinazotoa elimu ya awali kwa kuwapatia mafunzo  walezi na wazazi wa watoto hao  juu ya nanma ya kuwasaidia watoto wao kuwa wenye afya nzuri.

“Ni lazima tuweke mikakati juu ya kuwasaidia watoto wa namna hiyo hasa katika masuala ya lishe lakini si kila wakati wazazi na walezi wanaelewa somo la lishe au chakula,”anasema.

Anasema kumpatia mtoto fursa ya kuchagua vyakula wanavyokula wakiwa na umri mdogo kwa kuwapatia nafasi ya kuchagua vyakula vya afya vya aina mbili, inaweza kusaidia kutoa mwongozo utakaowasaidia kula vema.

“Hii inaweza kuwasaidia kupunguza hatari ya wao kukataa kula kitu chochote kabisa na hujihisi wao ndio wenye kauli ya mwisho.

“Wakati tunapowanyima watoto wetu fursa ya kuchagua chakula wanachokipenda, huwa wanahisi hawana la kufanya na huwafanya kuwa wenye hasira,” anasema Mtaalamu huyo.

 Daktari wa masuala ya lishe ya watoto mkoa wa Simiyu, Dk. Chacha Magige anakiri kuwa si rahisi kila mara hasa kama mtoto ni mwenye kupenda kuchagua chakula.

Amesema kuanza na mabadiliko ya taratibu ya chakula unachompatia inaweza kupumpunguzia shinikizo ambalo baadhi ya watoto huwa nalo saa za mlo zinapokaribia na kuepusha malumbano wakati wa chakula.

“Ni muhimu wawe na chakula ambacho unafahamu kuwa wanakipenda, lakini pia unaweza kuanzisha kitu kipya kwenye sahani yao ya chakula kwa pamoja.

Dk. Chacha alibaini mbinu ambayo ilikuwa nzuri ya kumshawishi binti yake mwenye umri wa amiaka mitatu ambaye awali alikuwa anakula Soseji tu na viazi vya kukaangwa(chips).

“Ilikuwa tukimlisha vyakula vingine anavitupa sakafuni au anavipuuza na matokeo yake hali chochote,” anasema Dk. Chacha.

Lakini anasema kwa kumshawishi kula kiwango kidogo cha chakula kipya mara kwa mara, sasa mwanae anakula karibu kila kitu.

“Ninasema, ‘Unaweza kumwambia, kula mara moja tu ujaribu na kama hautakipenda , unaweza kula chakula kingine. 

“Unahitaji kuwa mwenye subira kwa hiyo ikiwa watakataa, jaribu tena mara nyingine,” anasema Dk.Chacha.

Naye, Sesy Kenani ambaye ni mzazi katika mji wa Maswa anasema kuwa mzazi kuwa mfano mzuri kwa mtoto tangu akiwa na umri mdogo ni jambo muhimu.

“Kama unakula chakula cha afya wewe mwenyewe, mtoto wako ana uwezekano mkubwa wa kujifunza kutoka kwako kwa kuiga kile unachokifanya,” anasema.

Anaongeza kuwa kula pamoja wakati wa chakula au kuwasaidia watoto wadogo kuwaiga tabia ya ‘ulaji wa wazazi ‘ ni muhimu

Anasema kuwa ni muhimu kwa wazazi kutokizungumzia vibaya au kutoa maoni hasi juu ya chakula ambacho hawakipendi mbele ya watoto wao, kwani wanaweza kushawishi mtizamo wao juu ya vyakula vipya

Kutoa zawadi na kuwasifu watoto kwa kula vyakula vya afya inaweza kuimarisha tabia nzuri ya mtoto .

Hata hivyo, anasisitiza kuwa zawadi haipaswi kuhusiana na chakula, na badala yake mtoto apewe zawadi ya kutembelea sehemu za michezo, kuchora au kupanga vichezeo vya michoro ya vitu mbali mbali kwa mpangilio unaotakiwa.

Aidha amesema kuwa kila  mara  kwa mzazi kuepuka kutoa rushwa mwanao.

“Usiseme kama ukila chakula hiki nitakupa chokoleti au ice cream kwasababu hilo huwafanya kufikiria kuwa chakula cha afya tunachotaka wale kina thamani ndogo kuliko zawadi unayowapatia,” anasema.

Hasa kwa watoto wakubwa, chakula na uzito wa mwili huwa ni mada ambayo ina utata kidogo kuizungumzia na hofu juu ya muonekano wa umbo lao la mwili huchangia katika suala la kujiamini.

Utafiti wa hivi karibuni ulibaini kuwa unene wa mwili wa kupindukia na afya ya akili vina uhusiano wa karibu sana, huku watoto wanene kupita kiasi wakiwa na uwezekano mkubwa wa kuathirika kisaikolojia mfano kuwa na wasiwasi na kujihisi hawana raha wala matumaini.

Hivyo ni vizuri wazazi wabadili namna wanavyozungumzia chakula kwa kuepuka kuhusisha ulaji wa chakula cha afya na muonekano wa umbo la mwili wa mtoto.

“Watie moyo kuwa wenye afya kwasababu inawafanya wajihisi vizuri, badala ya kuwaeleza kuwa chakula wanachokula kitawafanya wawe na muonekano fulani,” anasema.

Pia anakubali kuwa lugha ni muhimu unapozungumzia suala la uzito wa mwili.

Alisema kuwa  muhimu familia zishauriwe kufanya mabadiliko kwa ujumla ili mtoto asijihisi kuwa analengwa kwa kupewa chakula fulani .

“Tujitahidi tuwe familia yenye afya, inamaanisha kuwa mtoto huenda asiwe na wazo kuwa wazazi wana hofia unene wao wa mwili  lakini hilo linaweza kuboresha lishe,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles