Na Sidi Mgumia, Morogoro
Katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya ardhi yanayofanywa na binadamu, dunia imeiona haja ya kuendesha biashara ya hewa ukaa (Carbon trading).
Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha utafiti wa Hewa Ukaa (NCMC) Profesa Eliakimu Zahabu, amebainisha uwapo wa biashara hiyo kwenye warsha ya siku moja iliyokutanisha Wanahabari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).
Prof. Zahabu alisema uanzishwaji wa biashara ya hewa ukaa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema biashara hiyo inahusisha upandaji na utunzaji wa miti, kuweka mifumo inayodhibiti uzalishaji wa hewa ukaa katika shughuli mbalimbali katika sekta za miundombinu, nishati, viwanda na kilimo.
“Biashara ya hewa ukaa inasisitizwa na Umoja wa Mataifa kwa sababu kiwango cha hewa ukaa kimeongezeka na kinatishia uhai wa viumbe hai” alisema Prof Zahabu
Biashara ya hewa ukaa ni mfumo na kusudi lake kubwa ni kupunguza gesi joto inayotokana na shughuli za viwanda na uchomaji wa uoto na ukataji wa miti.
Biashara hii ni maalum kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira na kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha Prof. Zahabu alibainisha kuwa pamoja na kuanzisha biashara hiyo, lakini pia zipo njia kadhaa za kukabiliana na uzalishaji wa hewa ukaa, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka, jijini Dar es Salaam na upandaji wa miti kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Usimamizi wa Mazingira katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Deo Shirima amesema ili kufanikisha biashara hiyo ni lazima kutimizwa kwa vigezo vya kimataifa.
“Miradi hii inahitaji rasilimali za kutosha, zikiwemo fedha na tafiti za kina lengo likiwa ni kukidhi viwango vya kimataifa vinavyosimamia biashara hiyo,” amesema mtaalam huyo wa mazingira.
Akifungua warsha hiyo Mkuu wa Chuo cha Misitu, Wanyamapori na Utalii, SUA, Prof Suzana Augustino alisema mpango huo unatoa wito kwa nchi wanachama kupunguza Gesi Joto (GHGs) katika anga ambazo ndizo sababu ya mabadiliko ya tabianchi.
Alibainisha kuwa athari za mabadiliko tabianchi ni pamoja na kuongezeka kwa ukame na mafuriko ya mara kwa mara, uhaba wa chakula na maji, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama Malaria na Homa ya Bonde la Ufa (RVF), kuyeyuka kwa seruji kwenye milima mirefu na kwenye ncha za Dunia na vile vile kutoweka kwa visiwa vidogo.
Aidha lifafanua kuwa kuna juhudi za kitaifa na kimataifa za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi. Moja ya mipango hii ni biashara ya kaboni (hewa ukaa). Biashara ya kaboni ya misitu ilikuwa inawezekana tu kupitia sera ya maendeleo safi (yaani Clean Development Mechanism (CDM) ya Itifaki ya Kyoto ya UNFCCC ambapo shughuli za upandaji miti mipya zinaruhusiwa.
Licha ya kuwa na eneo kubwa la misitu, Tanzania haikupata miradi ya CDM ya kupanda miti chini ya Itifaki ya Kyoto kwa sababu ya ukosefu wa utaalam na teknolojia. Hata hivyo, kupitia Mkataba wa Paris wa Desemba 2015, uhifadhi wa misitu ya asili umetambuliwa rasmi na nchi wanachama wa UNFCCC kuwa sera mpya ya kupunguza tatizo la mabadiliko ya tabia nchi. Sera hii inajulikana kama MKUHUMI – Mkakati wa Kupunguza Upotevu na Uharibify wa Misitu (REDD+).
Prof. Suzana alisisitiza kuwa Tanzania ina fursa ya kufaidika na utekelezaji wa MKUHUMI na sera zingine zinazojitokeza. Faida za kushiriki kwenye MKUHUMI ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa misitu nchini, uwezekano wa kupata pesa kutoka kwenye vyanzo anuwai vya kimataifa kama Mfuko wa Geen Climate Fund (GCF) na Mfuko wa Forest Carbon Partnership Facility (FCPF).
Pia, ushiriki katika MKUHUMI utaleta: teknolojia, vifaa, kujenga uwezo na utekelezaji katika miradi ya kupunguza Gesi Joto na ukuaji wa uchumi.
Mnamo Aprili 2008, Serikali za Norway na Tanzania zilitia saini Barua ya Kusudi la Ushirikiano katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi; kwa lengo la kuisaidia Tanzania katika mchakato wake wa kuwa tayari na MKUHUMI. Nchi hizi zilikubaliana kushirikiana kwa miaka mitano (2008-2013) ambapo Norway, iliahidi kutoa hadi Dola za Marekani milioni 100 kwa kipindi hicho. Hata hivyo, Tanzania haikukamilisha mchakato wake wa kuwa tayari na MKUHUMI, bado kulikuwa na maswala kadhaa ambayo hayakutimizwa, kama vile kuanzishwa kwa mfumo wa Kupima, Kuwasilisha na Kuhakiki takwimu (MRV), Utayarishaji wa Takwimu Rejea za Misitu (FREL) na kukamilisha Mfumo wa Kulinda Maslahi ya Utoaji wa Habari (yaani Safeguard Information System).
Kwa hivyo, Serikali ilianza utekelezaji wa mradi wa "Kuanzisha Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu wa Hewa Ukaa cha Tanzania" (yaani National Carbon Monitoring Centre – NCMC) tarehe 1 Januari 2016 kufuatia msaada wa Dola za Marekani milioni 4.2 kutoka kwa serikali ya Norway. Madhumuni ya mradi huo ilikuwa kuanzisha mfumo wa Kupima, Kuwasilisha na Kuhakiki takwimu (MRV) na Utayarishaji wa Takwimu Rejea za Misitu (FREL). Hivi sasa, mradi huu uko kwenye kipindi cha nyongeza ya mwaka mmoja na nusu (kuanzia Januari 2021).