33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kafulila: Nitapambana na mwanasiasa atakayevuruga pamba

Na Derick Milton, Simiyu

“Nikiwepo hapa Simiyu kama Mkuu wa Mkoa, hakuna Siasa wala Mwanasiasa ambaye atafanya siasa zake ili kuvuruga zao la pamba na akafanikiwa…labda nisiwepo, kama zilikuwepo basi… lakini huu ni mwisho wake”

Ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila ambayo ameitoa leo kwenye kikao cha wadau wa zao la pamba mkoani humo ambacho kilikuwa maalumu kujadili mpango mkakati wa zao hilo.

Hatua hiyo ya Mkuu wa mkoa, imekuja baada ya wadau wa zao hilo wakiwemo wanunuzi, Bodi ya pamba kulalamikia wanasiasa kuvuruga zao pindi inapowekwa mikakati ya kuboresha zao hilo.

Moja ya malalamiko kwa wanasiasa wa mkoa huo, ni kupinga sheria ya bodi ya pamba ambayo inawataka wakulima kabla ya kuanza kulima zao hilo wanatakiwa kuondoa masalia shambani na kuyachoma.

Lengo la utaratibu huo ni kupambana na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao wamekuwa wakishambilia zao hilo, ambapo moja ya visababishi ni kutokuodoa kwa masalia.

Malalamiko mengine ambayo yalielezwa kwenye kikao hicho ni mkoa wa Simiyu kukosa kitalu cha kuzalisha mbegu bora za pamba, licha ya kuwa kinara katika uzalishaji wa zao hilo nchini.

Wanasiasa wanalalamikiwa kuwa chanzo cha kuondolewa kwa kitalu hicho ambacho kilikuwepo katika Wilaya ya Meatu mkoani humo na kupelekwa mkoani Katavi bila ya sababu za msingi huku wakulima wakiangaika kupata mbegu bora.

Kutokana na sababu hizo Mkuu huyo wa Mkoa ameonekana kukerwa na hali hiyo na kutoa onyo kali kwa wanasiasa mkoani humo, kuwa hakuna mwanasiasa ambaye atafanikiwa kuvuriga mipango ya zao la pamba mkoa.

“Mwanasiasa yeyote ambaye atafanya siasa za kuvuruga pamba nitapambana naye, hatofanikiwa ikiwa mimi ni mkuu wa mkoa huu, Ni aibu kinara wa kuzalisha pamba nchini hatuna kitalu kwa sababu ya siasa za kijinga ambazo hazina msingi,” amesema Kafulila.

Amesema kuwa hakuna mwanasiasa ambaye atafanikiwa ikiwa yeye ataendelea kuwa kuu wa mkoa huo, huku akibainisha kuwa mwanasiasa yeyote ambaye atafanya siasa ambazo hazina tija kwenye pamba hatofanikiwa.

Mbali na hilo, amesema kuwa katika msimu ujao wa zao hilo, hakuna mnunuzi wa pamba ambaye atapewa kibali cha kununua zao hilo ikiwa hatawekeza katika kuongeza tija kwenye zao hilo.

Amesema kuwa wakulima wa zao hilo wanatakiwa kusaidiwa, hivyo amewataka wanunuzi wote kuhakikisha wanawekeza kwa kuwasaidia wakulima elimu ya kununi bora za kilimo, pembe jeo, mitaji ili waweze kuzalisha kwa tija.

“Wanunuzi mjiandae mapema, kama wewe hautawekeza kwenye pamba msimu ujao, hautapata kibali cha kununua pamba, tunataka kila mdau apambane katika kuongeza tija kwenye zao hili ili wakulima watoke kwenye umaskini,” amesema Kafulila.

Kwa upande wake Katibu Chama Cha Wanunuzi wa pamba nchini, Boaz Ogolla, amempongeza Mkuu huyo wa mkoa kwa uhamuzi wake wa kuwataka wanunuzi wote kuwekeza kwenye pamba na siyo kununua tu.

“Kwa hatua hii wakulima watasaidiwa kila sehemu na wataweza kuongeza tija kwenye pamba yetu, tatizo wengi wamekuwa wakinunua tu, lakini kwa hatua hii tunapongeza na sisi tunamuunga mkono ili kwenda kuboresha zao la pamba,” amesema Ogolla.

Katika mpango mkakati huo mkoa wa Simiyu umejipanga msimu ujao wa zao hilo 2021/22 kufikisha kilo laki tano katika uzalishaji wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles