Na Derick Milton, Busega
Wahenga walisema hujafa, hujaumbika, ndivyo unaweza kusema kwa familia hii ya Josiha Athuman (58) na mkewe, Suzana Ndekeja (35).
Wawili hawa wakazi wa kijiji cha Mayega kata ya Kalemela Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wote hawaoni (vipofu), wamebahatika kupata watoto wanne ambapo watatu kati ya hao nao ni vipofu na mmoja tu ndiye mwenye uwezo wa kuona.
Watoto wao ni Kwigema Matulala (14,), Yohaya Mayala (10), Sostenes Zabron (3.5) ambao wote watatu wanaulemavu wa kuona na mtoto nne ambaye ndiye pekee amekuwa tumaini ni Tumaini Lukasi (6).
Tumaini kama lilivyojina lake ndiye pekee amekuwa msaada wa familia hii licha ya kuwa ni mdogo.
Maisha yao
Kwa miaka zaidi ya 10 wanandoa hao wameishi kwa pamoja kama Mume na Mke baada ya kufunga ndoa, na walikutana wote wakiwa na tatizo la kutoona wakiwa kwenye harakati ya kuomba omba jijini Mwanza.
Athuman ambaye ni Baba wa familia hiyo anasema kwa muda wote ambao ameishi na mkewe na hata kujaliwa kupata watoto hao wanne, maisha yao yamekuwa yakitegemea kuomba mtaani.
“… nina wakati mgumu na familia yangu, kwani maisha ya familia yangu ni kuomba omba asubuhi hadi jioni, tumekuwa tukienda maeneo mbalimbali wakati mwingine tukivuka na kwenda kwenye miji mbalimbali kama Mwanza, Bariadi, Musoma, Tarime na hata Kahama kwa ajili ya kuomba ili kuweza kufanikisha mkate wetu wa kila siku na mahitaji yetu muhimu ya kibinadamu tukiwa na watoto wetu,” anaeleza Athuman.
Athuman anabainisha kuwa yeye hakuzaliwa na tatizo la kutoona, ispokuwa kwa mke wake Suzana ambaye yeye alizaliwa akiwa haoni.
Ilikuwaje kwa Athuman?
Akieleza namna alivyokumbwa na changamoto hiyo ya kutoona, Athuman anasema kuwa alianza kuugua macho yote mawili wakati akifanya biashara zake huko Ukerewe mkoani Mwanza.
“Wakati nafanya biashara zangu uko wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, lilianza tatizo kwenye jicho moja kuugua, baadaye likafuata jingine, licha ya kutibiwa sehemu mbalimbali ilifika hatua ikashindikana nikawa kipofu,” anaeleza Athuman kwa sauti iliyojaa huzuni kubwa.
Athuan anasema kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa yeye kujishughulisha na biashara zake kwani watu aliowaamini kuwa wangeweza kumsaidia kuendeleza shughuli hizo walimsaliti na kuzika biashara zake palepale.
Anasema licha ya kuhangaika huku na kule kwa ajili ya kusak matibabu lakini hakuna alivyofanikiwa na hivyo kujikuta akiikubali hali yake hiyo na kuamua kuingia mtaani kuishi maisha ambayo hakuyafikiria hapo awali.
“Baada ya kupata tatizo hilo Biashara zote ambazo nilikuwa nikifanya hazikuendelea tena, kwani watu ambao niliwaweka wanisaidie waliniibia hadi mtaji kuisha, ndipo nilipoanza maisha ya kuomba omba mtaani jijini Mwanza,” anaeleza Athuman.
Athuman anasema kuomba huko ndio ilikuwa aina mpya ya maisha yake ndani ya mkoa huo wa Mwanza kazi ambayo aliifanya kwa kipindi kadhaa kabla ya kukutana na mwenzi wake wa maisha ambaye amekuwa naye kwenye shida na raha kiduchu.
Kwa mujibu wa Athuman, wakati akiendelea na shughuli hiyo jijini Mwanza, alifanikiwa kumpata Suzana ambaye naye alikuwa anaomba, na kwamba hiyo ilikuwa ni baada ya kuomba siku moja msaidizi wake ampeleke katika Kijiji cha Nyaluhande kilichoko Busega mkoani Simiyu, ambapo huko ndiko ulikuwa mwanzo wa wao kuwasiliana baada ya kubadilishana namba za simu.
Mawasiliano yakaanza
Athuman anasema kuwa; “Nilipofika Nyumbani nilimpigia simu, tukaongea…nilimwambia kuwa mimi nataka nikuoe licha ya wote kuwa na ulemavu wa macho, nataka tukaishi pamoja, alinikubalia akanipeleka kwao kunitambulisha kisha tukafunga ndoa ya kimila baada ya kulipa mahali,” anasema Athuman.
Kutokuona si changamoto kwao
Athuman anasema kuwa suala la kutoona kwao siyo changamoto, kwani kazi zote za ndani wamekuwa wakifanya kwa kusaidiana na wamekuwa wazifanya kama watu wenye macho yanayofanyakazi ambao wanaona.
Kwa mujibu wa Suzana, changamoto kubwa ni wao kuendelea kuomba omba mitaani wakiwa na watoto wao, lakini pia kukosa nyumba ya kuishi pamoja na kiwanja ikiwa pamoja na kutokosa mradi wa kuwaletea kipato.
“Sisi kwetu kuwa vipofu siyo tatizo hata kidogo, maana kazi zote za ndani tunafanya vizuri sana bila ya tatizo, changamoto yetu tunapenda kuona ni lini tutaacha hii kazi ya kuombaomba, lakini pia watoto wetu tuwapeleke shule,” anasema Suzana.
Suzana anasema kuwa wamehangika sana kwenye ofisi za serikali ikiwemo kwa Mkuu wa Wilaya, Maendeleo ya Jamii kuomba wapewe mkopo ili waweze kuanzisha mashine ya kusaga na kukoboa nafaka kwa ajili kuendesha maisha yao na imeshindikana.
“Nimezunguka sana serikali lakini hakuna msaada hata kidogo, tuliwaambia watusaidie mashine tu sisi ya kukoboa na kusaga nafaka inatutosha, hatutaki biashara nyingine maana tunajua tutaibiwa, lakini hii ya mashine tutafanya wenyewe na tunaweza kuisimamia lakini hakuna msaada,” anaeleza Suzana.
Haki ya elimu
Athuman na Suzana licha ya kuhitaji msaada wa kujengewa nyumba, kupewa mashine ya kusaga na kukoboa nafaka, wanasema kuwa hitaji lao kubwa la kwanza ni kuona watoto wao wanaenda shule kama watoto wengine.
“Hatupendi hata kidogo kila siku tunaenda kuomba omba na watoto wetu, kama Baba yao nimekuwa naumizwa sana na hili jambo, hakuna mtu yeyote hata serikali wa kunisaidia hili jambo,” anaeleza Athuman.
Wanasema kuwa wamekuwa wakiangaika sana kuona watapa wapi msaada wa kuwasomeshea watoto wao kwenye shule maalum mkoani Mwanza, lakini imeshindikana licha ya kwenda hadi serikalini.
“Tumekuwa tukiangaika sana hata kwa mkuu wa mkoa, Maendeleo ya jamii, watusaidie hata nauli pekee ili hawa watoto tuwapeleke shule uko Misungwi Mwanza kwenye shule zao maalumu wapate elimu kama watoto wengine,” anaeleza Athuman.
Athuman anasema kuwa licha ya kuhangaikia watoto wao waende shule hakuna msaada wowote ambao wamepata kutoka serikali hata kwa viongozi wa Wilaya na Mkoa, ambapo anapaza sauti kuomba watoto wake wapelekwe shule.
Anasema kuwa yeye kama Baba wa Familia na Mke wake, hawana uwezo wa kuwapeleka shule, kwani licha ya kutokuwepo kwa ada mahitaji madogomadogo kama sare na vingine hawana uwezo wa kuvipata.
“Tuliomba watusaidie basi hata nauli tu tuwapeleke hivyo hivyo lakini walisema hawana, hivyo tunaomba Mtanzania yeyote mwenye uwezo atusaidie kuwapeleka watoto wetu hawa shule,” anaeleza Athuman.
Wamlilia Magufuli
Wawili hao wamemuomba Rais Dk. John Magufuli, kuwasaidia watoto wao waweze kupata elimu kama ilivyo kwa wengine, kwani wana imani ikiwa watoto wao watapata haki hiyo wataweza kuja kuwa msaada mkubwa kwao.
“Tumekuwa tukimsikiliza Rais Magufuli anavyosaidia watu wengine, tunamuomba na sisi atusaidie, kwa wasaidizi wake huku wameshindwa kwani tumehangika kuomba msaada hata mdogo lakini wameshindwa, tunamuomba Rais wetu atusaidie hawa watoto waweze kwenda shule,” aneleza Suzana.
Mbali na hilo wanaomba kusaidiwa mkopo wa mashine ya kusaga kwa ajili ya kujipatia kipato, ikiwa pamoja na kujengewa nyumba kwani ambako wanaishi kwa sasa siyo kwao wamehifadhiwa kwa ndugu.