Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM
MAJI mengi yanayotokana na visima virefu na vifupi vilivyochimbwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, si salama kwa afya za watumiaji.
Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) pamoja na mambo mengine yanasisitiza kuwapo na huduma bora za maji na usafi wa mazingira.
Katika utafiti uliopewa jina la ‘Tathmini ya Mahitaji ya Maji katika Jiji la Dar es Salaam kulingana na upatikanaji kwenye vyanzo’ ulifanywa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) na Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala mbalimbali ya kijamii (CCI).
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Meneja Miradi wa CCI, Mwanakombo Mkanga, alisema ulihusisha kata za Vingunguti, Tungi, Mtoni na Manispaa ya Temeke.
“Tulijikita kuangalia mtazamo wa jamii katika kuboresha huduma za maji safi na taka, ubora wa vyoo bado ni dhaifu katika maeneo mengi na utapishaji ni changamoto kwa sababu maeneo mengi hayafikiki kiurahisi,” alisema Mkanga.
Alitoa mfano kuwa licha ya ofisi za Serikali za mitaa kutoa vidonge vya kutibu maji, baadhi ya watu wanaouza maji wamekuwa wakikaidi kuviweka na wengine wakitoa sababu mbalimbali zikiwemo za matenki kuwa juu.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Wilbard Kombe, alisema Jiji la Dar es Salaam linakuwa kwa haraka lakini kasi ya ukuaji wake haiendani na huduma za maji na usafi wa mazingira.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, kuna wadau wengi wamejitokeza kutoa huduma, hivyo kuna haja ya kuwa na mfumo utakaoshirikisha watoa huduma wasio rasmi ili kutoa huduma bora.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Maji, Wilson Mshuba, alisema wana mkakati wa kudhibiti uchimbaji holela wa visima ambao utaanza kutekelezwa katika Wilaya ya Temeke.
“Kuna tatizo kubwa katika uchimbaji visima, katika maeneo mengi umaliziaji wake huwa hauwi mzuri. Hivyo kwa yeyote anayetaka kuchimba kisima tunamshauri aje wizarani apate maelekezo ili hata kama anataka kuchimba sehemu zilizozungukwa na vyoo, tumuelekeze aweze kupata maji mazuri,” alisema Mshuba.