Na Javius Kaijage
KWA siku za hivi karibuni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati wamekutana nchini DRC ili kujadili kitisho cha ugaidi wa kimataifa unaoonekana kulinyemelea bara la Afrika hususan ukanda wa Jangwa la Kusini mwa Sahara.
Hatua ya mataifa ya Rwanda, Uganda, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) kukutana mjini Kinshasa kujadili kitisho hiki, ni baada ya kuwepo tetesi kuwa kundi linalojiita dola la Kislamu (ISIS) tayari limeishatua nchini DRC.
Inasemekana kundi hili hatari la dola la Kiislamu baada ya kufurushwa kwa nguvu kutoka katika makazi yake ya Irak na Syria limeamua kujitanua katika mataifa ya Afrika ambako linaamini haliwezi kupata upinzani mkali kivita.
ISIS ikiwa DRC imekuwa ikishirikiana na makundi ya waasi yaliyodumu kwa muda mrefu yakiwemo ya Allied Democratic Forces (ADF) kuishambulia nchi hiyo.
Kundi la uasi la ADF ambalo limedumu zaidi ya miaka 20 nchini DRC huku likifanya mauaji ya kutisha, inasemekana linaendelea kupata nguvu baada ya kupata msaada wa kifedha na rasilimali watu kutoka kundi la kigaidi la ISIS.
Si tu Dola la Kislamu limejikita katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pekee, bali pia kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari inaonekana kundi hili ni chanzo kikubwa cha mauaji ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara nchini Msumbiji.
Juni 4, mwaka huu kundi hili la ISIS limekiri kufanya mashambulizi huko Msumbiji Kaskazini katika Jimbo la Cabo Delgado.
Ni kweli kwa miaka kadhaa tumekuwa tukisikia kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa kundi hili la ISIS liko katika nchi za Afrika Magharibi zikiwemo za Mali na Burkina Faso, lakini kusikika pia kwamba liko katika nchi za DRC na Msumbiji hakika ni kitisho kikubwa kwa taifa letu.
Nasema ni kitisho kikubwa kwa taifa letu la Tanzania kwa maana ya kwamba kijiografia nchi za Msumbiji na DRC ni majirani zetu wa karibu hivyo mwingiliano wa watu kutoka pande hizi katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii lazima uwepo.
Hata hivyo hakuna sababu ya watanzania kuogopa, kwani mara zote vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimekuwa chachu ya kuwaletea wananchi usingizi mnono usio na shaka.
Pamoja na majeshi yetu ya kuwa na viwango vya juu sana katika medani za kivita bado kuna sababu ya kutoridhika na mafanikio haya kwani ugaidi wa karne hii hufanyika kisayansi na kwa mikakati mikubwa sana.
Magaidi mamboleo ambao kimsingi hawana sare za utambulisho, huwezi kuwabaini kwa maneno, matendo na hata hisia zao kwani mara nyingi sura zao huonyesha upole na ukarimu kwa lengo la kutimiza kusudio lao.
Magaidi ni viumbe wa ajabu sana kwani kwao kutumia maneno ya Mungu kinyume kutoka katika vitabu vitakatifu ili kujitoa mhanga kufanya maangamizi ya kutisha kupitia kujilipua, kuua kwa mtutu wa bunduki au kuchinja ni jambo la kawaida.
Ni viumbe wa kushangaza kwani mbali na kuyapotoa maneno matakatifu ya Mola, bado huendeleza vitendo vya utekaji kwa vijana wa kiume, watoto wa kike, mabinti na wanawake.
Sasa ni nini kifanyike? Cha kufanya ni wananchi kutoa taarifa mapema iwezekanavyo katika sehemu husika mara wasikiapo au kuona viashiria vya uhalifu huu kwani majeshi yetu yanao uwezo, nia na sababu ya kupambana na ugaidi kwa kishindo.