23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAJASUSI WAIHUSISHA URUSI NA USHINDI WA TRUMP

Donald Trump
Donald Trump

WASHINGTON, MAREKANI

SASA ni dhahiri kwamba Urusi ilifanya mbinu chafu za kimtandao kufanikisha ushindi wa mgombea wa urais wa Marekani kupitia Chama cha Republican, Donald Trump.

Mashirika ya kijasusi ya Marekani yametoa taarifa kwa magazeti makubwa ya hapa, kwamba Urusi kwa usiri mkubwa ilifanya mbinu kumsaidia Trump kushinda urais Novemba 8, mwaka huu.

Ripoti iliyotolewa kwa gazeti la New York Times, inasema mashirika ya kijasusi yana ‘imani kubwa’ juu ya ushiriki wa Urusi kudukua taarifa wakati wa uchaguzi ambao Trump alimshinda mgombea wa Democrat, Hillary Clinton kupitia kura za wajumbe, maarufu kama ‘electoral college’.

Hata tathmini iliyofanywa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), iliyoripotiwa katika gazeti la the Washington Post, ilitoa majibu kama hayo.

Hata hivyo kama ilivyotarajiwa, timu ya Trump imekanusha taarifa hizo za CIA ikisema: “Hawa ndio watu walewale waliosema Saddam Hussein (rais wa zamani wa Irak) alikuwa na silaha za maangamizi.”

Maofisa wa Urusi wamekuwa wakikanusha taarifa hizo za udukuzi.

Ijumaa iliyopita, Rais Barack Obama aliamuru uchunguzi ufanyike juu ya madai ya kuwapo kwa udukuzi wa kimtandao wakati wa kipindi cha uchaguzi, yanayowahusisha maofisa wa Urusi.

Udukuzi huo unadaiwa kuzilenga baruapepe za chama cha Democratic na msaidizi muhimu wa aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Hillary Clinton.

Mwezi Oktoba mwaka huu, maofisa wa Serikali ya Marekani waliinyoshea kidole Urusi wakiishutumu kwa kuingilia utaratibu wa kampeni za uchaguzi.

Taarifa zinasema wadukuzi wa Urusi walijipenyeza mfumo wa kompyuta wa kamati ya taifa ya chama cha Republican na vilevile mfumo wa kompyuta wa chama cha Democrat, lakini hawakuweka wazi taarifa walizodukua kutoka mitandao ya chama cha akina Trump na Mike Pence.

“Kwa mujibu wa taarifa za mashirika hayo ya kijasusi, Warusi walipenyeza taarifa za chama cha Democrat kwa mtandao wa WikiLeaks,” ilisema taarifa iliyoandikwa na gazeti la New York Times.

Wanachama wa Democrat walichukizwa pale barua pepe za akaunti ya kamati ya taifa ya chama chao na zile za mwenyekti wa kampeni za uchaguzi za chama hicho, John Podesta, zilipodukuliwa.

Kipindi fulani wakati kampeni zikiwa zimepamba moto, Trump alionyesha waziwazi kuiunga mkono Urusi katika mchakato wake wa kudukua barua pepe za Hillary.

Wa-Democrat walidai kuwa udukuzi ule ulikuwa ni kitendo cha makusudi cha jaribio la kuzihujumu kampeni za mgombea wao wa urais.

Maofisa wa Ikulu ya Marekani walisema Rais Obama alitaka uchunguzi ufanyike haraka kabla ya kukabidhi madaraka Januari 20, 2017.

Democrat walikuwa na wasiwasi kwamba huenda Trump akiingia madarakani atakuwa hana muda wa kulishughulikia jambo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles