Na DERICK MILTON-SIMIYU.
WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Kilimo kuendelea kuchukua hatua, ikiwemo kuvifuta vyama vya ushirika vinavyokiuka sheria kanuni na taratibu za uendeshaji.
Alisema Serikali itaendelea kuingilia kati usimamizi wa vyama hivyo ili kuhakikisha vinawanufaisha wanachama wote na siyo baadhi ya watu.
Majaliwa alitoa maagizo hayo jana, wakati wa hafla ya siku maalumu ya kuhamasisha ushirika, iliyofanyika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu ambako kunaendelea maonesho ya sikuu ya wakulima kitaifa (Nanenane) ambapo aliwakilishwa na Waziri wa Nchi, ofisi wa Waziri Mkuu Uwekekezaji, Agela Kairuki.
Alisema amepata taarifa ya Wizara ya Kilimo mpaka sasa zaidi ya vyama vya ushirika 3,317 vimefutwa kutokana na kuna na matatizo mbalimbali, ikiwemo ubadhilifu wa mali za vyama hivyo.
Aliitaka wizara kuhakikisha hatua hizo zinaendelea kuchukuliwa ili kuwepo na vyama ambavyo vinawanufaisha wananchi.
“Niwapongeze sana wizara ya kwa hatua ambazo wamezichukua za kufuta vyama zaidi ya 3,317, endeleeni kuchukua hatua hizo, ni bora tubaki na vyama vichache ambavyo vinafanya vizuri kuliko kuwa na vyama vingi ambavyo havitimizi malengo yake,” alisema Majaliwa.
Alimtaka waziri kuhakikisha hatua zaidi kali zinaendelea kuchukuliwa kwa vyama ambavyo bado vimeendeea kufanya ubadhilifu wa mali na pesa za wakulima.
Alisema Serikali haitavumilia hata kidogo kuona mali na fedha za wanaushirika zinaendelea kuwanufaisha watu wachache badala ya wanachama.
Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kurudisha mali kwenye baadhi ya vyama ambazo zilichukuliwa na watu wachache.
“ Kwa miaka mitatu tumerudisha mali za vyama vya ushirika zaidi ya vinne, ikiwemo SHIRECU, NYANZA, KCU na KDCU, ombi langu kwa viongozi wa vyama hivyo hakikisheni mnatunza mali hizo na kuziendeleza,” alisema Majaliwa.
Aliwataka wanachama wa vyama vyote vya shirika nchini kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa fedha na taarifa mbalimbali mara kwa mara kwenye vyama vyao na siyo kuiachia serikali tu.
Alisema kuchelewa kufanya hivyo imeendelea kusababisha mali na fedha za wanachama kuendelea kuliwa na viongozi wa vyama hivyo kutokana na wao kushindwa kusimamia mapema.
Mrajisi Mkuu wa Vyama vya Ushirika,Dk. Benson Ndiege alisema bado ushirikia umeendelea kuwa na changamoto ya kuwepo kwa baadhi ya viongozi wasiokuwa waadilifu.