Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa amewaasa watanzania kulinda amani iliyopo kuvutia wawekezaji wengi nchinizaidi miongoni mwa sifa za Tanzania ni utulivu ambao ni kichocheo kikubwa cha ukuaji uchumi.
Kauli hiyo aliitoa juzi Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akitoa neno la shukrani kwa Mwenyekiti wa Mkutano wa 11 Baraza la Taifa la Biashaara Tanzania (TNBC) uliokutanisha wafanyabishara ambapo alisema uchumi unakua kwa kasi na wawekezaji wanavutiwa kuanzisha biashara mpya kutokana na hali ya utulivu.
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya amani na ukuaji kiuchumi na ndiyo maana kuna mzungumzaji mmoja kutoka Arusha alisema watalii wameongezeka nchini na kipato kimeongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisema
Majaliwa alimshukuru Rais Dk. John Magufuli ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo kwa kutoa nafasi kubwa kwa wafanyabishara na sekta binafsi kuzungumza masuala yanayowakwaza ili serikali itoe majibu muafaka na kupatikana njia sahihi ya kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
“Nashukuru ndugu rais ametoa majibu hapa hapa kwa baadhi ya malalamiko ya wafanyabiashara lakini naamini hawezi kumaliza yote hapahapa kwa sababu kuna mengine yanahitaji kujadiliana ndani ya vikao vyetu,” alisema Majaliwa.