Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania na wadau wa soka kuungana kuhakikisha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inafuzu kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar 2022.
Katika kikao chake na wadau wa Taifa Stars kilichofanyika leo Novemba 4, 2021 kwenye ukumbi wa uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, zimechangwa shilingi bilioni 1.6 ambazo zitatumika kuihudumia timu katika maandalizi ya mechi zilizobaki za kufuzu michuano hiyo.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Majaliwa amesema ni lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anakuza sekta ya michezo nchini na anataka kuona mafanikio katika timu za Taifa hivyo mikakati ya kuifanya timu ya Taifa ifanikiwe ni sehemu ya kutimiza malengo ya Rais.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda, taasisi za umma na binafsi na wadau wengine kuendelea kujitokeza kuichangia timu ya Taifa ili iweze kuweka historia ya kushiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza.
Wadau walioshiriki katika kikao hicho ni Taifa Gas, GSM, Azam, CRDB, NBC, Lake Oil, Star Oil, K4 Security, Kambiaso pamoja na wadau wengine.
Stars imeingia kambini kujiandaa na michezo ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo Novemba 11, na Madagasca Novemba 14,2021.