27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aitaka Sido kuwa na teknolojia rafiki

Na DERICK MILTON-BARIADI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lijielekeze katika kubuni teknolojia na mitambo rafiki inayolenga kutatua changamoto za wajasiriamali kulingana na mazingira yao.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za SIDO lakini bado kuna  changamoto za wajasiriamali wadogo ambazo lazima zishughulikiwe kwa kasi kubwa  kufungamanisha shughuli za SIDO na uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana alipofungua maonyesho ya SIDO   kwenye uwanja wa Nyakabindi mjini Bariadi  ambako wajasiriamali zaidi ya 500 wanahudhuria.

Alisema ili kufikia uchumi wa kati inambidi kila Mtanzania mahali alipo afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu.

“Tusipoteze wakati   kufanya mambo yasiyo na tija. Tuzingatie falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu.

“Mfano kwa hapa Bariadi, tunatarajia SIDO watuletee teknolojia na mitambo inayoweza kurahisisha ukamuaji wa mafuta yanayotokana na mbegu za alizeti na pamba, kwa Dodoma taknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata zabibu.

“Kigoma pelekeni teknolojia na mitambo kwa ajili ya kuchakata mbegu za michikichi na kwenye maeneo yanayolimwa korosho teknolojia na mitambo  ya kubangua korosho na maeneo kama Ilula ambayo yanazalisha nyanya kwa wingi wapate teknolojia na mitambo ya kusindika na kuhifadhi nyanya na mbogamboga,” alisema Majaliwa.

Alisema  ili nchi iweze kupata mafanikio, SIDO inatakiwa iwaunganishe wajasiriamali na taasisi mbalimbali za fedha  wapate mikopo yenye masharti nafuu.

“Mahitaji ni makubwa hivyo lazima SIDO ishirikiane na taasisi nyingine likiwamo Baraza la Uwezehaji Wananchi Uchumi. (NEEC),” alisema.

Waziri Mkuu aliwasihi wajasiriamali wanaoshiriki maonyesho hayo kutumia fursa hiyo kujifunza namna nzuri ya kuboresha viwango vya bidhaa zao na kubadilishana ujuzi na uzoefu, kupanua masoko na kubaini teknolojia zitakazorahisisha uzalishaji wa bidhaa.

‘’Kumbukeni kuwa Serikali ina matarajio makubwa katika sekta ya viwanda hususan katika kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,’’  alisema.

Awali,  alitembelea mabanda mbalimbali ya washirii wa maonyesho hayo yakiwamo ya taasisi za Serikali zinazotoa huduma katika sekta ya viwanda na biashara zikiwamo SIDO na Shirika la Viwango Tanzania  (TBS).

Nyingine ni Mamlaka ya Vyakula na Dawa (TFDA), Wakala wa Vipimo (WMA),  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan-Trade), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles