Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza maofisa kilimo waliopo makao makuu ya wilaya waondolewe na kupelekwa vijijini wakasaidie kulima mkonge.
Uzalishaji wa mkonge nchini umeporomoka kutoka tani 235,000 zilizokuwa zikizalishwa miaka ya 1960 hadi kufikia tani 36,000 zinazozalishwa kwa sasa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi jijini Tanga jana, Majaliwa alisema Serikali imeamua zao hilo na mengine yarudishwe kwenye hadhi yake ya uzalishaji.
Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya urejeshwaji wa mali za mkonge ambao pia ulikwenda sambamba na ufunguzi wa jengo la ofisi ya makao makuu ya Bodi ya Mkonge mkoani humo.
“Hakuna kukaa ofisini, peleka vijijini waende kulima mashamba, waende waliko wakulima wawasadie namna ya kuandaa shamba, kulima vizuri pamoja na masoko yake. Wakawasaidie mkulima mmoja mmoja, wakulima wa kati na wawekezaji,” alisema Majaliwa.
Alisema zao hilo lilikuwa linalimwa mikoa 12, hivi sasa linalimwa mikoa minne pekee ambayo ni Tanga, Morogoro, Pwani na Kilimanjaro.
“Miaka ya 60 Tanzania ndiyo ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji wa mkonge duniani, ilikuwa inazalisha zaidi ya tani 235,000 wakati mahitaji yalikuwa tani 550,000. Lilikuwa linatuletea fedha nyingi za kigeni kwa zaidi ya asilimia 65.
“Leo tunalizasha tani 36,000, ukiuliza kwanini hatuzalishi, hakuna sababu. Ardhi ipo, wanaotamani kulima wapo, Serikali ipo, uzalishaji tani 36,000,” alisema Majaliwa.
Alisema awali walianza kufufua mazao ya korosho, chai, tumbaku, pamba na kahawa na hivi sasa wameongeza mkonge na michikichi na kuitaka mikoa yote inayolima zao hilo ijipange vizuri.
MALI ZILIZOTOWEKA
Majaliwa alisema awali walipofanya utafiti waligundua si mkonge uliotoweka, bali hata mali zake zimetoweka na kwamba tayari wametembelea katika vyama vya ushirika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Kilimanjaro kuokoa mali hizo.
“Tumekuja Tanga, tunatoka hapa tunakwenda Corecu Pwani kuona mali hizi za wanaushirika wadogo ziko wapi, nani kachukua na kwenye zoezi hili hakuna mtu ataonewa, tunataka turudishe mali za wakulima wajenge imani na kilimo chao na ushirika wao.
“Mashamba yamechukuliwa kwa hila tu, mitambo ya kukamua mkonge, nyumba, kila kitu kitarudi, hakuna ujanja ujanja kwenye Serikali hii,” alisema Majaliwa.
Alitoa mfano wa jengo lililokuwa katikati ya Jiji la Tanga ambalo awali liliuzwa kwa Sh milioni 40, lakini tayari Serikali imelirudisha.
MKONGE SI NYUZI TU
Majaliwa alisema mkonge una faida nyingi kama kuzalisha pombe, gesi, mbolea, dawa za binadamu na mifugo na kuitaka Bodi ya Mkonge ifuatilie faida zote ili mkulima anufaike.
“Bei kwa tani moja ni zaidi ya Sh milioni 3.6, lakini mkulima alikuwa hapati fedha hizo, kila mkoa wenye ardhi nzuri na wananchi wanaotamani kulima Serikali iwape msaada walime.
“Awe mtu mmoja mmoja, bila kujali wa kati au mkubwa asaidiwe, akiweza eka moja, mbili alime. Wakulima wa kati, wakulima wakubwa walime zao hili. Ukipata mwekezaji kutoka popote waliopo ndani na wanaokuja wapokelewe wasaidiwe,” alisema Majaliwa.
UZALISHAJI TANI 120,000
Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alisema wameanza mikakati mbalimbali ya kufufua zao hilo kwenye mikoa 12, wataanza na mitano ili kuongeza uzalishaji ndani ya miaka minne kufikia tani 120,000 kutoka 36,000 za sasa.
“Tumejipanga vizuri na baadaye tutakwenda kwenye mikoa mingine kama Shinyanga, Simiyu, Mwanza ambayo katika utafiti imeonyesha inakubali zao za mkonge ili turudi kwenye nafasi yetu ile ya miaka ya sitini ambayo tulikuwa tunaongoza,” alisema Mgumba.
UMMY
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Ummy Mwalimu, alisema amehamasika kulima na tayari ameanza na hekta 7.5 katika Kijiji cha Nkale Kata ya Kwamatuku, Halmashauri ya Handeni Vijijini.
“Nilipata shida ya mbegu, ni gharama kweli, nikachukua maoteo mkonge wake naambiwa hauna ubora, sasa waziri nimeshindwa kununua hizi ambazo zina ubora Mtanzania wa kawaida atawezaje… lengo langu ni kulima hekta 50,” alisema Ummy.
WAKUU WA MIKOA
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, alisema wakulima wako tayari kulima mkonge, lakini gharama za uzalishaji ni kubwa na kuiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), isaidie kuwakopesha wakulima.
Alisema kwa sasa zao hilo linalimwa na kampuni kubwa na kwa mwaka 2019/20 wamezalisha tani 2,136 na kutoa ajira zaidi ya 1,200.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata ole Sanare, alisema wilaya mbili mkoani humo zinajihusisha kulima zao hilo na hadi sasa wana ekari 19,834.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alisema zao hilo linalimwa wilaya za Mwanga na Same na kwamba wana wawekezaji watatu, hawana wananchi wenye mashamba madogo madogo.
Aliiomba Wizara ya Kilimo ijikite kusaidia wakulima katika tafiti zinazohusiana na zao hilo kwani uzalishaji umekuwa ukifanywa na raia wa nje zaidi kuliko wenyeji na kusababisha wengi kuliona zao hilo kama geni.