25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi watakiwa kuendelea kupiga nyungu

Na AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM 

WANANCHI  wametakiwa kuendelea kujifukiza kwa kutumia miti na mimea ya asili, ikiwemo mwarobaini ili kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya alitoa rai hiyo Dar es Salaam jana na  kueleza  mti wa mwarobaini hauna madhara yoyote, bali ni mti wenye manufaa kwa tiba asili/mbadala ya magonjwa mbalimbali.

Alisema  kumekuwepo na upotoshaji katika baadhi ya mitandao ya jamii ambayo ilimnukuu  kwa kusema mti wa mwarobaini  haufai kujifukiza kwa sababu  una kemikali  zenye sumu jambo ambalo si kweli.

“Mti wa mwarobaini unatibu magonjwa arobaini, majani yake  yanatumika kutibu minyoo, magamba yanatumika kutibu homa na mafuta ya mti huu yanatumika kutengeneza sabuni kwa ajili ya ngozi, mti huu ni mzuri na una manufaa makubwa kwa jamii yetu”, alisema.

Alisema taasisi yake ilifanya utafiti kupitia maandiko mbalimbali na kupata njia mbili za kumpa nafuu mtu mwenye maradhi mbalimbali na kutaja njia hizo kuwa ni dawa lishe ambayo ina virutubishi  vinavyoweza kujenga na kuimarisha kinga ya mwili kupambana na virusi na kumfanya mtu apone.

Alitaja njia ya pili kuwa ni kujifukiza kwa kutumia mimea au majani ya miti mbalimbali ambayo husaidia kufunguka kwa mishipa ya damu, kufungua kifua kinachobana  pamoja na kuondoa uchovu na msongo wa mawazo.

“Mimea mingi ina mafuta tete (essential oil), hivyo harufu mbalimbali za majani ya miti yanaingia haraka mwilini na hivyo kusaidia kufanya mwili kutulia, kifua kufunguka na lile joto linasaidia mishipa ya damu kufunguka na kufanya mfumo wa hewa kuwa mzuri kwenye mwili wa mtu, na aina hii ya tiba imetumika miaka mingi barani Afrika,” alisema Profesa Mgaya.

Alisema  katika utafiti huo, NIMR ilipata idadi ndefu ya majani ambayo yanatumika na wananchi hususani Tanzania na makabila mbalimbali, na hivyo walishauriana kuweka makundi matatu na endapo mtu atapata mmoja wa mmea mmoja wapo anaweza kujifukiza.

Alitaja kundi la kwanza ni mkaratusi, kivumbasi (kashwagala) na mchaichai, kundi la pili ni karafuu (mbegu), tangawizi na limau (majani) na kundi la tatu alisema ni mwarobaini na mpera na kusisitiza kuwa wakati wa kujifukiza joto lisiwe kubwa  na muda usizidi dakika kumi kwa watu wazima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles