Derick Milton, Simiyu
Waziri mkuu kassimu Majaliwa, ameziagiza benki zote ambazo zimetoa pesa kwa wafanyabishara wa zao la pamba kwa ajili kununua zao hilo kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa mikoa ni wafanyabishara gani wamepewa na kiasi gani.
Majaliwa amesema kuwa kuna hofu kuwa baadhi ya wafanyabishara waliopewa pesa hizo wanaweza kuzitumia katika mambo mengine wakati nia ya pesa hizo ni kununua pamba tu na kuhakikisha inatoka kwa wakulima.
Amesema kuwa serikali kupitia benki kuu tayari imeshughulikia tatizo la zao hilo, ambapo baadhi ya wanunuzi wamepewa pesa za kununua pamba na wameanza kununua.
Amewataka wakulima kuwa wavumilivu na kwamba pamba yote ambayo ipo kwa wakulima itanunuliwa na wakulima kulipwa pesa zao kwa ajili ya kufanya shughuli zao nyingine ikiwemo kujiandaa na kilimo hicho kwa msimu mpya.
“Ninaziagiza benki zote ambazo zimetoa pesa kwa wanunuzi wa pamba, toeni taarifa kwa wakuu wa mikoa ni wanunuzi gani wamepewa na kiasi gani na wakuu wa mikoa hakikisha mnawasimamia ili pesa hizo ziweze kwenda kwa wakulima wa pamba tu,” amesema.
Aidha amewaagiza wakuu wa mikoa kusimamia pesa zinazopelekwa kwa wakulima kwa kuweka ulinzi ili kuwe na usalama na wakulima waweze kulipwa ipasavyo.