KAIMU Mhasibu Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Sezari Semfukwe, amedai kuwa Mhifadhi Mkuu wa zamani wa mamlaka hiyo, Benard Murunya, aliidhinisha hundi ya malipo na dokezo la safari ya Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Semfukwe alidai hayo jana mjini hapa, wakati alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Murunya na wenzake watatu ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka.
Akiongozwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, Hamidu Sembano aliyesaidiana na Wakili Mwandamizi Rehema Mteta, shahidi huyo alidai mbele ya Hakimu Patricia Kisinda wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha kuwa Murunya alikuwa pia akishirikiana na Shad Kiambile.
Shahidi huyo wa kwanza, alitoa kumbukumbu ya kitabu cha malipo kinachoonyesha hundi za malipo yenye namba 309/0238 ya Septemba 9, 2011 iliyokuwa na dokezo la safari kutoka kwa Murunya kwenda kwa Kiambile aliyekuwa Kitengo cha Fedha.
Katika ushahidi huo, alitoa kumbukumbu nyingine ya hundi ya malipo iliyokuwa ikionyesha imelipwa dola za Marekani 66,890 kwa Kampuni ya usafirishaji ya Cosmas.
Alidai hundi za malipo namba 310/0379 ya Oktoba 29, 2011 na Transformer Invoice namba 5609 ya Septemba 7, 2011 zenye thamani ya dola za Marekani 66,890 zililipwa kwa Antelope Tours & Traveling kwa ajili ya tiketi za Murunya, Muyungi na Maige.
Aliendelea kudai mahakamani hapo kwamba kumbukumbu ya kitabu cha malipo, inaonyesha hundi namba 2758 na 002755 ya Septemba 9, 2011 ililipwa kwa Kampuni ya Cosmas Travelling Agent na ilisainiwa na Murunya na Kiambile.
Wakati shahidi huyo akitoa vielelezo hivyo ili vitumike kama ushahidi wa kesi, mawakili wa washtakiwa wakiongozwa na Wakili Amani Mirambo waliomba kujua ni vielelezo vya aina gani upande wa mashtaka vimepangwa kuwasilishwa.
Kutokana na kuibuka kwa mvutano huo wa kisheria, Hakimu Kisinda aliahirisha kesi kwa muda ili kuwapa nafasi mawakili wa utetezi kuafiki endapo vielelezo hivyo vipokewe kama kielelezo, hatua ambayo mawakili hao walikubaliana nayo na vielelezo kupokewa.
Hakimu Kisinda aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 24, mwaka huu, huku akiutaka upande wa Serikali kuhakikisha wanaleta mashahidi wengi.
Watuhumiwa hao walisomewa maelezo ya awali wakidaiwa kuhusika na matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha mamlaka upotevu wa dola za Marekani 66,890 ambazo ni sawa na Sh 133,780,000.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wengine ni Meneja Utalii wa NCAA, Veronica Funguo, Meneja Utalii wa NCAA na Mkurugenzi wa Kampuni ya Cosmas, Salha Issa.