25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MAHIGA ATUMIE UZOEFU WAKE KUSAFISHA HALI YA HEWA

 

TANGU kuasisiwa kwa taifa la Tanzania, limejijengea heshima kubwa katika medani za kimataifa kutokana na msimamo wake.

Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alifanya jitihada kubwa kuing’arisha nyota ya taifa hili huko nje.

Msimamo wake usiotetereka katika kusimamia misingi ya haki na utu, ilifanya aheshimike hata na mataifa makubwa.

Katika mikutano mbalimbali ya kimataifa, watu walipenda kusikiliza ujumbe kutoka Tanzania.

Nchi yetu ilikuwa moja ya waasisi wa umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote wakati wa vita baridi.

Msimamo wa Mwalimu Nyerere kutoruhusu mataifa makubwa kuichagulia Tanzania marafiki, ndio uliofanya taifa letu liheshimike zaidi duniani.

Ni kwa kutumia msimamo huo wa Mwalimu ndio uliofanya huko nyuma nchi yetu kuwa na uhusiano na nchi kama Korea Kaskazini (DPRK) ingawa imekuwa na mivutano isiyoisha na Marekani tangu miaka ya 1950.

Hata hivyo, si msimamo wa Tanzania kuwa na uhusiano wowote na nchi ambayo imetengwa na karibu dunia nzima.

Ndiyo maana tunasema tamko la Serikali kukanusha Tanzania kuwa na uhusiano wa aina yoyote ile, ukiwamo wa kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa au kijeshi na Korea Kaskazini, iliyowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (UN), lina umuhimu mkubwa.

Msimamo huo wa Tanzania ulitolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, kujibu ripoti ya hivi karibuni ya Baraza la Usalama la UN, inayoituhumu Tanzania kukiuka vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Korea Kaskazini.

Dk. Mahiga alisema ripoti hiyo imeituhumu Tanzania kuendeleza uhusiano wake na Korea Kaskazini katika mambo fulani ambayo hakutaka kuyataja.

Pamoja na kwamba imekuwa ni msimamo wa taifa letu kutokubali kuchaguliwa marafiki, busara haiitumi Tanzania kuendelea kuwa na uhusiano na Korea Kaskazini, nchi ambayo UN imeiwekea vikwazo vya kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa, kijeshi na mawasiliano ya kila aina ili kuitenga, baada ya kukiuka agizo la kusitisha utengenezaji na majaribio ya silaha za nyuklia.

MTANZANIA Jumapili tunaamini kwamba Dk. Mahiga atakapoenda makao makuu ya UN hivi karibuni, atatumia fursa hiyo kuiambia dunia kwamba Tanzania ilishakata uhusiano na Korea Kaskazini muda mrefu.

Hatuna shaka na Dk. Mahiga kwamba atatumia ubobezi wake katika mambo ya kimataifa kusafisha hali ya hewa.

Bila shaka Dk. Mahiga atalisaidia taifa kufafanua kwamba uhusiano wa kidiplomasia uliokuwapo miaka ya nyuma sasa upo katika ngazi ya chini mno.

Tanzania hairuhusu kuchaguliwa marafiki na nchi nyingine. Hata hivyo nchi yetu ina imani kwamba, kuwapo kwa silaha za maangamizi ni tishio kubwa kwa amani, si tu katika rasi ya Korea, bali duniani kote.

Ni kweli nchi yetu haina ugomvi na Korea Kaskazini, lakini tunapendekeza iendelee kuungana na mataifa mengine duniani kuishawishi nchi hiyo kuachana na silaha za nyuklia kwani si kitendo kizuri kwa heshima ya ustaarabu na usalama wa dunia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles