Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, amesema lazima mikakati ya uhamiaji inayoeleweka ianze kuwekwa wakati nchi ikiwa inaelekea katika uchumi wa mafuta na gesi.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana alipofungua mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya (EU) na wale wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Dk. Mahiga alisema mkutano huo ulikusudia kujadili mfumo wa uchumi, masuala ya uchaguzi katika nchi zao, tishio la uvunjifu wa amani na wahalifu wa kimataifa.
“Sasa hivi kuna wimbi la vijana wa Afrika ambao katika kutafuta maisha wanakimbilia Ulaya, limejitokeza mara nyingi na hata hapa Tanzania kuna vijana wanapita kwenda nchi nyingine wanasema wanazamia.
“Lakini suala hilo haliishii hapo, ipo siku Tanzania itakuwa na utajiri wa mafuta na gesi, watu watakuja kwa maana hiyo ni lazima tuanze kuweka mikakati ya uhamiaji inayoeleweka na Wazungu tunawaambia kuliko waache watu watumbukie baharini au wafe Jangwa la Sahara, tufanye mkakati wa maendeleo utakaofanya vijana wetu watulie huko nyumbani.
“Tunawaambia wao toka nchi zilizoendelea wana wajibu wa kutusaidia sisi, wasiwe tu wanasema hili ni tatizo letu na kwa jinsi wanavyokataa kuwapokea wahamiaji na wakimbizi Serikali zao zinawafikisha mahali watu wanakataa wageni,” alisema Dk. Mahiga.
Pia alisema ni lazima pawe na mkakati wa kuzuia migongano na mifarakano kati ya nchi na nchi.
“Tunajadiliana tunawezaje kutumia nafasi zetu kuzuia mifarakano na si kusubiri matatizo yatokee bali kuyazuia pawe na mazungumzo kati ya nchi hizo,” alisema Dk. Mahiga.