31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ripoti: Wawili kati ya watano hawajui kusoma, kuandika

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa
Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

WATU wawili kati ya watano wa miaka zaidi ya 15 walioingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini sana wamebainika hawajui kusoma na kuandika.

Watu hao walibainika baada ya utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) iliyohusisha kaya 7,480 ambazo kati ya hizo 5,440 zilitoka Tanzania Bara na 2,040 zilitoka Zanzibar.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa matokeo ya Tathmini ya Kaya Masikini, Mtaalamu wa Utafiti kutoka NBS, Reina Kiama, alisema lengo la tathmini hiyo ya awali ni kuonyesha taswira ya wanufaika wa mpango katika hatua ya awali, kupima uwiano kati ya kundi la wanaopata ruzuku na wasiopata ikiwa ni pamoja na kutathmini namna utambuzi wa kaya masikini ulivyofanyika.

Reina alisema kulingana na tathmini iliyofanyika katika elimu, walibaini kuwa kiwango cha wasiojua kusoma na kuandika katika kaya za mpango kipo chini ukilinganisha na zile zenye umasikini wa kawaida, pia kiwango cha uandikishaji wa shule kwa watoto wa miaka saba hadi 13 ni asilimia 72 huku wale wa miaka 14 hadi 17 ikiwa ni asilimia 51 tu hali inayosababishwa na ukosefu wa fedha kwa asilimia 39 na umbali ni asilimia 11.

Kuhusu afya, alisema walibaini kuwa uchunguzi wa afya kwa watoto ni asilimia ndogo na kati ya watoto 10 wanaozaliwa sita huzaliwa katika vituo vya afya huku mmoja kati ya wanne waliozaliwa hai hawakupata huduma baada ya kuzaliwa kwa kipindi cha wiki nane wakati kwa upande wa wajawazito wakipata huduma mara moja tu kabla ya kujifungua.

“Uchunguzi wa afya kwa watoto chini ya miaka mitano ni mdogo na kwamba tulibaini asilimia 23 tu ndio hupelekwa kwa mtoa huduma za afya na asilimia 90 walibainika kuwa wanaumwa huku asilimia 58 walibainika kuwa hawapelekwi kwa watoa huduma za afya pindi wanapoumwa na hiyo inatokana na ukosefu wa fedha, lakini pia asilimia 32 inaonyesha kuwa inatokana na sababu za mila na desturi potofu,” alisema Reina.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa, alisema tathmini hiyo iliangalia idadi ya watu kiumri, elimu, afya, kipato na matumizi katika kaya zilizofanyiwa tathmini kwa pande zote.

Dk. Chuwa alisema asilimia 51 ya kaya 7,400 zilizopo katika mpango huo zinaongozwa na wanawake ambao kwa kawaida umasikini wa mahitaji ya msingi ni mkubwa kuliko zile zinazoongozwa na wanaume.

“Ni matumaini ya Serikali kuwa watakapofanya tathmini nyingine katika kaya hizi na kuzifuatilia tutaona mafanikio makubwa ya kupunguza hali ya umasikini,” alisema Dk. Chuwa.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa WB, Bella Bird, alisema Tanzania itakuwa kielelezo katika dunia na Afrika kutokana na mafanikio iliyopata katika mpango huo.

Alisema mpango huo unatakiwa kuigwa na wataendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha wanafanikisha malengo yake.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ikulu, Peter Ilomo, alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inapunguza umasikini hadi ifikapo mwaka 2030 na matokeo ya tathmini hiyo yatachukuliwa kwa uzito.

“Serikali imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi wake na nyie ni mashahidi kutokana na mambo mbalimbali ambayo yameshafanyika,” alisema Ilomo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles