NA MWANDISHI WETU
MAHAKAMA ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, imezuia mwili wa mfanyabiashara maarufu wa madini wa Arusha, Jubilate Benjamin Ulomndugu, kuzikwa mpaka kifo chake kitakapochunguzwa kwa kina na maofisa wa Jeshi la Polisi na madaktari.
Ndugu wa karibu wa marehemu wanapinga anayedaiwa kuwa mke wa marehemu, Zainabu Rashid, kufanya mazishi ya mumewe kwa madai kuwa hakuwa mke halali wa ndoa.
Hata hivyo, mahakama hiyo mbele ya Hakimu Devotha Msofe imezuia ndugu wa marehemu kufanya chochote kuhusiana na mali za marehemu hadi shauri mama litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Jubilate alifariki dunia Januari 15, 2019 katika Hospitali ya Aga Khan Nairobi, Kenya na baadaye kuhamishiwa Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa huduma ya mazishi lakini maziko yake hayakuweza kufanyika baada ya mke huyo kupeleka mgogoro huo mahakamani baada ya ushauri uliotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Katika hati yake kinzani ya kupinga kesi iliyopo mahakamani, mmoja wa ndugu zake marehemu, Onesy Benjamin Ulomi, amekanusha kuwa Zainabu Rashid, ambaye ndiye mwombaji katika shauri hilo, kuwa mke wa sheria wa marehemu na amemtaka athibitishe ukweli huo.
“Jubilate Benjamin Ulomi alikuwa mdogo wangu na hakuwa na kwa uelewa wangu hakuwahi kufunga ndoa ya sheria na mwombaji,” anadai Onesy, ambaye ni miongoni mwa walalamikiwa wanne katika shaurio hilo.
Hayo anayaeleza katika kiapo chake kilichowasilishwa mahakamani na wakili wake, Joseph Ngiloi kutoka kampuni ya uwakili wa Makoa Attoneys.
Walalamikiwa wengine katika mgogoro huo ni Werandumi Benjamin Ulomi, Awadi Ulomi na Abdulrasul Ulomi.
Anadai Jubilate ambaye alikuwa ametengana na kanisa lake kwa kuwa na watoto wengi na wanawake tofauti bila kufuata mwongozo wake wa roho, aliungana tena katika kanisa lake baada ya toba mbele ya Mchungaji Chambulila wa Kaniasa la Msamaria Mwema (Good Samaritan) na akasema kuwa hakuwahi kuwa na ndoa yoyote iliyosajiliwa.
Onesy amedai baada ya kupitia maombi yaliyopo mahakamani amebaini maombi yaliyoletwa hayana mashiko yoyote kwa vile hayajaungwa mkono na maombi yoyote ya awali ambayo yanaweza kuangaza ushahidi wa masuala ya msingi kuthibitisha amri zitakazolewa kesi mama itakaposikilizwa.
Baada ya kutoa zuio hilo, Mahakama iliamuru shauri hilo litajwe Februari 7 mwaka huu. Katika hati yake ya kuunga mkono maombi yake, mwombaji anasema alikuwa mke halali na wa sheria wa Jubilate na waliishi pamoja kama mume na mke kwa miaka 12.
Anadai walibarikiwa kuwa na watoto wawili na walitengana kwa muda isivyo halali, lakini alibakia kuwa mke wa sheria wa marehemu hadi tarehe ya kufa kwake. Mwombaji ameeleza kuwa baada ya kufariki dunia mume wake, Januari 18, 2019, pande zote mbili zilikutana kukubaliana juu ya njia bora za mazishi.
Mwombaji anadai hata Januari 19, 2019, kila kitu kilibadilishwa na walalamikiwa pamoja na ndugu zake wengine wa ukoo na kuzuia mwili wa marehemu kuchukuliwa Merelani kama moja ya mila yao, kitendo ambacho kilimwongeza shaka juu ya nini kilichokuwa chanzo ya tatizo hilo.
Anadai Onesy alitoa maelekezo kwa watumishi wa sehemu ya kuhifadhia miili ya marehemu kwamba hakuna mtu anayepaswa kuruhusiwa kuona mwili huo, hali ambayo ilimlazimisha kuandika barua kwa Mkuu wa Wilaya kuomba msaada wake.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya alimshauri kutafuta taratibu za mahakama kwa kuwa ofisi yake haikuwa na mamlaka ya kutatua suala hilo.
Hapo ndipo mwombaji alipoamua kukimbilia mahakamani kutafuta haki zake juu ya mgogoro huo.