Na KULWA MZEE
-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuonya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kwa kutokufika mahakamani mara mbili.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa alitoa onyo hilo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai kesi ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa upande wa mashtaka lakini mshtakiwa hakuwapo.
“Ni rai ya upande wa Jamhuri kwamba mahakama iukumbushe upande wa utetezi kuwa mshtakiwa Lissu ni wakili mzoefu na kwamba utaratibu wa kuomba udhuru mahakamani unafahamika na uzingatiwe,” alidai.
Hakimu Mwambapa alisema hiyo ni mara ya pili kwa Lissu kutokufika mahakamani kuhudhuria kesi yake hiyo ambako mara ya kwanza ilikuwa ni Julai 10, 2017 na jana.
Wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya alidai imetokea bahati mbaya lakini Hakimu Mwambapa alimueleza kuwa bahati mbaya mfululizo haiwezekani, hivyo akatoa onyo la mwisho.
Jamhuri iliomba kesi hiyo ipangwe tarehe ya karibu kwa ajili ya kusikilizwa na mahakama ilikubali na kupanga iendelee kwa kusikilizwa Agosti 22 mwaka huu.
Lissu anakabiliwa na kesi ya uchochezi akidaiwa akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alitoa kauli za uchochezi kuwa: “Mamlaka ya Serikali mbovu ni ya udikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote.
“Huyu diktekta uchwara lazima apingwe kila sehemu. Kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene”.
Wakati huohuo, kesi inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli imeahirishwa hadi Septemba 12,2017 kwa sababu Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo hakuwapo.